MALIASILI YAZIDI KUNG'ARA MWANZA YAITANDIKA TIMU YA NETBALL YA KATIBA NA SHERIA 38-8 SHIMIWI 2025

September 03, 2025


Na John Bera – Mwanza


Timu ya netiboli ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuonesha ubabe kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa kuichapa kwa kishindo Wizara ya Katiba na Sheria kwa mabao 38–8, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Timu hiyo ilianza kwa kasi na kutawala mchezo kutoka mwanzo hadi dakika ya mwisho, ikionesha uelewano mzuri, umakini mkubwa na nidhamu ya hali ya juu uwanjani. Ushindi huo umeiweka Maliasili katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye hatua za mtoano.

Kocha wa timu hiyo, Bi. Rehema Kapela, amesema ushindi huo si wa bahati nasibu, bali ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu na ari ya wachezaji wake waliodhamiria kuweka historia mwaka huu.

“Tumekuwa tukifanya mazoezi kwa bidii na leo tumeona matokeo. Wachezaji wameonesha kujituma, umoja na uthabiti. Tuna malengo makubwa, na huu ni mwanzo mzuri kwetu,” alisema Kocha Kapela.

Mchezaji wa timu hiyo, Julia Kepha, ambaye aling’ara katika mchezo huo kwa kucheza kwa kiwango cha juu katika safu ya ulinzi, amesema walijiandaa kisaikolojia na kimwili kuhakikisha wanapata ushindi.

“Ushindi huu umetokana na kazi ya pamoja. Kila mmoja alitimiza majukumu yake. Tuliingia uwanjani tukiwa na malengo, na tulihakikisha tunayatimiza kwa vitendo,” alisema Julia.

Kwa upande wake, Kaimu  Mratibu wa Timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. George Rwezaura, amechukua fursa hiyo kuipongeza timu kwa ushindi huo wa kuvutia na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na benchi la ufundi kuhakikisha timu inasonga mbele zaidi.

“Leo tumeandika historia dhidi ya timu ngumu. Ushindi huu umetupa hamasa kubwa na tunawaahidi watumishi wenzetu kwamba tutapambana hadi mwisho. Hakuna majeruhi, morali ni kubwa, na tumejiandaa vyema kwa mechi zijazo,” alisema George.

Katika michezo mingine ya leo, timu ya wanaume ya Maliasili iliibuka na ushindi wa bao 2–0 dhidi ya Tume ya Haki za Binadamu kwenye mchezo wa kuvuta kamba, huku timu ya wanawake ikipoteza kwa bao 1–0 dhidi ya timu ya Mkoa wa Geita (RAS Geita).


Kesho michezo hiyo itaendelea kwa timu Kamba ME kukutana na RAS Pwani na Kamba KE kukutana Maji wakati Netball watacheza na TAMISEMI

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »