Dar es Salaam, Septemba 8 2025:
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imekamata kilogramu 33,077.623 za dawa za kulevya aina mbalimbali huku ikiwashikilia watuhumiwa 940 kuhusika kwenye matukio tofauti ya uhalifu wa dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, akizungumuza na waandishi wa Habari leo Septemba 8,2025 jijini Dar es Salaam, amesema, pamoja na dawa hizo, pia zimekamatwa, kilogramu 4,553 za mbegu za bangi, silaha mbili za moto aina ya gobore na bastola zikiwa na risasi 11, magari tisa, pikipiki 26 na bajaji mbili zilizohusishwa kwenye uhalifu huo na kuteketeza ekari 64 za mashamba ya bangi
Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam katika mtaa wa Tupendane uliopo Manzese walikamata watu watatu akiwemo raia wa Lebanon wakiwa na kilogramu 2.443 za dawa za kulevya aina ya Cocaine zilizoingizwa nchini kutokea nchini Brazil kupitia nchini Kenya hadi Uganda kwa njia ya kumezwa na baadaye Tanzania kwa njia za vipenyo.
Katika tukio lingine amesema, jijini Dar es salaam, kwenye klabu ya “Bad London” iliyopo Temeke kwa Azizi Ally na klabu ya “Sanaa” katika eneo la “Reggae bar” iliyopo Masaki, walikamata sigara za kielektroniki (e cigarette) pisi 50 zilizotengenezwa kwa bangi zenye ujazo wa mililita 10 kila moja.
Sigara hizo za kielekroniki zilizotengenezwa kwa kutumia kemikali pamoja na skanka ziliingizwa nchini kutokea Uingereza. Miongoni mwa Kemikali hatarishi kwenye bangi hizo ni pamoja na THC, benzene na madini ya cadmium, lead, na mekyuri.
"Kemikali hizo pamoja na madhara mengine ya kiafya, huweza kusababisha magonjwa ya akili, saratani, kuharibu mimba kwa mama wajawazito, kuathiri maendeleo ya ukuaji wa mtoto akiwa tumboni, kusababisha udumavu wa akili baada ya mtoto kuzaliwa na hivyo kuathiri uwezo wa kujifunza pamoja na uraibu." alisema Kamishna Lyimo.
Katika eneo la “Bahari Beach” amesema, walikamatwa raia wa Marekani na mke wake raia wa Tanzania wakiwa na chupa 11 za dawa ya kulevya aina ya Ketamine pamoja na bangi na hatua za kisheria zinaendelea dhidi yao.
Vilevile, kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi jijini Dar es salaam,walikamatwa watu wanne kwa kukutwa na kilogramu 10.37 za mirungi wakiwa kwenye hatua za kuisafirisha kwenda nje ya nchi huku ikiwa imefichwa kwenye vifungashio vyenye chapa ya bidhaa za chai, kwa lengo la kukwepa kubainika.
Kadhalika, kupitia mifumo ya ufuatiliaji ya kimataifa katika kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu kutumika kutengeneza dawa za kulevya,Kamishna Jenerali Lyimo amesema, Mamlaka ilizuia uingizaji nchini lita 69.8 za kemikali aina ya Methyl ethyl ketone (MEK) na Ephedrine ambazo zilikuwa ziingizwe hapa nchini kinyume na taratibu.
Pia, kupitia operesheni zilizofanyika mkoani Mara, alikamatwa mhalifu kinara wa uzalishaji na usafirishaji wa bangi aitwaye Masero Ryoba Muhabe (44) akiwa na tani 6.5 za bangi. Kwa muda mrefu, Muhabe amekuwa akijihusisha na uzalishaji na biashara ya bangi wilayani Tarime mkoani Mara na kusafirisha ndani na nje ya nchi.
Katika tukio lingine mkoani humo, alimkatwa Simoni Gervas Mkonda (51) akiwa na kilogramu 193 za bangi pamoja na silaha aina ya bastola ikiwa na risasi 11 ambayo amekuwa akiimiliki kinyume cha sheria na kuitumia kulinda biashara zake haramu.
Aidha, mkoani Mbeya,waliwakamata Henry Shao (36) na Veronika Samumba (31) wakiwa na biskuti 241 zilizotengenezwa kwa mazao ya bangi. Watajwa ni wahandisi na wafanyakazi wa kampuni binafsi za ujenzi za HSS Engineering Company Limited na JIC Company Limited za jijini Mbeya.
"Baada ya upekuzi eneo la mtaa wa Forest watuhumiwa walikutwa na vifaa wanavyovitumia kutengeza biskuti hizo na kueleza kwamba wateja wao wakubwa ni wahandisi na vijana wa vyuo na mitaani." alisema Kamishna Lyimo
Pia, mkoani Mwanza amesema walikamata watuhumiwa sita wakiwa na kilogramu 452 za dawa za kulevya aina ya bangi zikisafirishwa kwa gari aina ya Skania lenye namba za usajili T 384 BWN likiwa na tela namba T.602 ANQ mali ya kampuni ya CocaCola ya Nyanza iliyopo Mwanza pamoja na bajaji mbili zilizokuwa zinabeba bangi hizo kutoka kwenye gari tajwa.
Vilevile, kupitia operesheni zilizofanyika katika mikoa ya Mara, Tabora, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Tanga, Ruvuma na Morogoro, zilikamatwa kilogramu 25,919.8 za bangi, mirungi, skanka na Heroine,
Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya, inaendelea kuvunja mitandao ya dawa za kulevya na kubaini mbinu mpya za biashara na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo, kuongeza wigo wa utoaji elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, lengo likiwa ni kuakisi dhamira ya Taifa katika kulinda usalama wa wananchi na kuimarisha uchumi, kujali utu, kulinda afya za watanzania, hatimaye kuimarisha ustawi wa Taifa letu.



EmoticonEmoticon