Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema maamuzi ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kisasa pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari nchini, yamekuwa na tija kwa kuongeza ufanisi na uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam, kuhudumia tani milioni 27.7 kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 kutoka uwezo wa awali wa kuhudumia tani milioni 18 mwaka 20212022.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Agosti 22, 2025, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus Abed, amesema kiwango hiki cha uhudumiaji wa Shehena ni ukuaji wa Asilimia 15 kwa mwaka na hakijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Bandari hiyo.
Bw. Gallus amesisitiza kuwa tangu kuingia kwa waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam Kampuni za DP WORLD na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) mwaka mmoja uliopita, uwezo wa Bandari hiyo kuhudumia shehena umeongezeka kwa Tani milioni 4, kutoka kuhudumia tani milioni 23.69 mwaka 2023/2024 hadi kufikia kuhudumia tani milioni 27.7 mwaka 2024/2025.
Pia ametoa rai kwa Wateja na Wadau wa TPA kupitia Bandari ya Dar es Salaa, kuendelea kuitumia Bandari hiyo, kutokana na kutoa huduma kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa kiwango kikubwa ili kwa pamoja kufikia malengo yao na Taifa kwa Ujumla.
EmoticonEmoticon