📍 Apita makanisani kuwaomba waende kupiga kura, kulinda Amani ya nchi
📍 Padre James wa mtaa wa Mdote, asema kura inakomesha mashindano
📍 Aomba Oktoba 29 wapewe kipaumbele wawe wa kwanza kupiga kura
📍 Mchungaji kiongozi James Ngereza aombea uchaguzi ufanyike kwa Amani
📍 Asema nchi ikichafuka wananchi hawawezi kufanya ibada
Na Mwandishi Wetu, Muheza
MGOMBEA ubunge Jimbo la Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA ameshiriki ibada ya Jumapili katika makanisa ya Aglikana na kanisa la Nazareth yaliyopo wilayani Muheza na kutumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi wa dini kuliombea Taifa na kuwahamasisha waumini wao wakapige kura Oktoba 29.
MwanaFA alisema lengo la kufika katika makanisa hayo, ni kuwahamasisha waumini wajitokeze kwenda kupiga kura Oktoba 29 kwa amani ili watumie haki yao ya kikatiba ya kuwachagua wagombea wanaowapenda.
Mgombea huyo alipita katika kanisa la Anglikana doyosisi ya Tanga la Mtakatifu Raphael lililopo mtaa wa Mdote mjini hapa ambapo alisema kila mtu ajitokeze kushiriki zoezi la kupiga kura kwakuwa ni haki ya kila mtu kwa wale waliojiandikisha.
Alisema Taifa linatambua umuhimu wa wananchi kufanya ibada katika mazingira ya amani hivyo wakati huu wa kuelekea kufanyika uchaguzi Mkuu ni muhimu waumini hao wakaliombea ili kusitokee machafuko kwasababu zozote zile.
"Tuombee Taifa letu liendelee kuwa na amani, pasipokuwa na amani hatuwezi kufanya ibada kila mtu atakuwa anakimbia, ni wajibu wenu viongozi wa kanisa mkatumia ibada zenu kuliombea Taifa na kuwasihi waamini wenu wajitokeze kwenda kupiga kura," alisema.
MwanaFA aliyekuwa ameongoza na mgombea udiwani wa kata ya Majengo Muccadam Abbas pamoja na Katibu wa UVCCM wilaya ya Muheza Ajuaye Msigala, alisema kuwa Taifa la Tanzania limejengwa katika misingi ya Umoja na mshikamano na watu wake hawabaguani kwa tofauti za kidini wala kabila hivyo Amani ya nchi itailindwa kwa gharama yoyote kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema uchaguzi ni suala linalotakiwa lisiwe na mjadala kwasababu ni haki ya kikatiba ya mtu ambaye amejiandikisha kutumia haki hiyo kwenda kupiga kura kwa amani ili kuchagua viongozi wake watakaodumu kwa kipindi cha miaka mitano.
"Ndugu zangu nimekuja kuwahamasisha Oktoba 29 mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura mkachague viongozi wenu," alisema na kuongeza,
"Sikuja hapa kufanya kampeni wala kuomba kura bali nawaaambia CCM imemsimamisha Dkt Samia Suluhu Hassan kugombea nafasi ya Urais, Mimi nimegombea ubunge Jimbo hili la Muheza na ndugu Muccadam Abbas amegombea udiwani wa kata hii ya Majengo,".
Padre wa kanisa Hilo la Anglikana mtaa wa Mdote Fr James Wazir alisema jukumu la kanisa mara nyingi wanapofanya misa za ibada huliombea Taifa pamoja na viongozi nchi iendelee kuwa na amani ili kila mtu afanye shughuli zake.
"Pasipo na amani, utulivu hatuwezi kukaa kama hivi tukafanya ibada, hivyo ni jukumu letu sisi kanisa kuombea amani ya nchi na viongozi wate," alisema Padre Wazir.
Alisema katika kitabu cha Biblia Zaburi ya 127 inaelezea hivi, "bwana asipojenga nyumba, waijengao hufanya kazi bure, bwana asipolinda mji yeye aulindae anakesha bure".
Padre Wazir alisema ni haki ya kila Mtanzania kwenda kupiga kura kuchagua viongozi na akaomba viongozi wa dini wapewe kipaumbele kwa kupiga kura wakiwa mstari wa mbele ili wakimaliza warudi kuwahudumia waamini wao.
"Sisi ni Watanzania ni haki yetu kwenda kupiga kura, Mithali sura ya 18 na Aya ya 18 inasema "kura hukomesha mashindano, hufuta maneno ya viongozi", twendeni tukapige kura na tuifanye nchi yetu iendelee kuwa na amani," alisema.
Naye mchungaji kiongozi wa kanisa la Nazareth James Ngereza aliwataka Watanzania kwenda kupiga kura kwa ajili ya kulinda Amani nchi na kamwe wasithubutu kuibagaza amani kwa namna yoyote Ile.
Alisema wao kama viongozi wa dini mara zote wamekuwa wakiomba kwa ajili ya Taifa ili kuhakikisha nchi inabaki na utulivu kwa faida ya vizazi vya Sasa na baadae.
"Nchi ikichafuka hakuna atakayefanya ibada kila mtu atakimbia kivyake, tulindeni amani na tutoke tukapige kura kwa faida kubwa ya amani ya nchi yetu," alisema Mch Ngereza.
EmoticonEmoticon