NGOs ZATAKIWA KUWAJIBIKA

August 11, 2025

 




Na WMJJWM-Dodoma


Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), yametakiwa kuwa wazi na kuwajabika katika utekelezaji wa majukumu yao hasa kuwahudumia wananchi kupitia miradi mbalimbali wanayotekeleza kwa maendeleo ya jamii. 

Hayo yamesemwa leo Agosti 11, 2025 na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakati akifungua Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2025 linalofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kuanzia Agosti 11-13.

Naibu Waziri Mwanaidi ameeleza kwamba uwazi na uwajibikaji wa Mashirika hayo ndiyo msingi wa kutambuliwa kwa mchango wao katika maendelo ya Taifa. 

“Viongozi na wasimamizi wa miradi ya kimaendeleo ya uchumi katika mashirika yenu nawaomba kuzingatia uwajibikaji, pamoja na kuwa tayari kubadilishana uzoefu miongoni mwa Mashirika ili kuwa na maendeleo endelevu kwa nchi yetu” amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Aidha amesisitiza kwamba kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanapaswa kutoa elimu ya kiraia kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia. 

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni nyenzo muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi, hivyo ameyaasa Mashirika hayo kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuhakikisha wananchi wananufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mwantum Mahiza amesema Bodi hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha NGOs zinafuata kanuni na taratibu zilizopo ili kufanikisha maono yao katika kuwahudumia wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Gasper Makala asema Baraza hilo limeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha Mashirika hayo yanashirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuwahudumia wananchi kupitia utekelezaji wa miradi.

Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2025 linaongozwa na kaulimbiu isemayo: Tathmini ya Miaka Mitano kuhusu Mchango wa NGOs katika Maendeleo ya Taifa 2020/2021-2024/2025: Mafanikio, Changamoto, Fursa na Matarajio.

MWISHO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »