KILIMANJARO YA SWEDEN YATWAA UBINGWA WA BONANZA LA SERENGETI NCHINI UBELGIJI

August 17, 2025

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Nyamanga, wakimkabidhi kombe la ubingwa wa Bonanza la Serengeti nahodha wa timu ya Kilimanjaro kutoka Sweden, Abbas Bachu, baada ya kushinda fainali ya michuano hiyo iliyofanyika jijini Antwerp, Ubelgiji, tarehe 15-16 Agosti, 2025.


Na Mwandishi Wetu, Antwerp, Ubelgiji.


Timu ya soka ya Watanzania iitwayo Kilimanjaro kutoka Sweden imetwaa tena kwa mara ya nne mfululizo ubingwa wa kombe la Bonanza la Serengeti katika michuano iliyofanyika tarehe 15-16 Agosti, 2025, jijini Antwerp, Ubelgiji.


Kilimanjaro ilitetea ubingwa wake baada ya kuifunga timu nyingine ya Watanzania kutoka Uingereza iitwayo Leeds Swahili mabao 2-1 kwenye mchezo mkali wa fainali. Magoli ya Kilimanjaro yalifungwa na Feisal Amir na Fryad Sabri huku la Leeds likifungwa na Murtaza Fuad. Hii ni mara ya tatu kwa timu hizi kukutana fainali.


Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Nyamanga, alimkabidhi kombe la ubingwa nahodha wa Kilimanjaro, Abbas Bachu, ambaye naye alimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, na kuibua shwange za washabiki wao. Kilimanjaro hushiriki ligi ya daraja la sita nchini Sweden katika mfumo wa madaraja saba.


Michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya nne tangu mwaka 2021 na kudhaminiwa na Benki ya NBC na kampuni ya ASAS, zote za Tanzania, huandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha Watanzania Ughaibuni, kukuza vipaji vya soka na kuitangaza Tanzania kimataifa. Mkurugenzi wa Diaspora kutoka Tanzania, Salvatory Mbilinyi; Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Chipeta; na Mabalozi wa Kenya, Sudan Kusini na Somalia nchini Ubelgiji nao walishuhudia.


Jumla ya timu 15 za Watanzania na watu wa Afrika Mashariki waishio barani Ulaya zilimenyana. Waandaaji Tanzania walikuwa na timu kumi kutoka Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Scotland, Ujerumani na Ufaransa huku Burundi ikiwa na timu tatu na moja moja kutoka Rwanda na Somalia.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »