DEVOTA MBURARUGABA NA SAMIRA AMOUR WAIBUKA KIDEDEA UCHAGUZI UBUNGE VITI MAALUM KURA ZA MAONI

August 01, 2025

 




Wa kwanza kulia ni Devotha Daniel aliyepata kura 1,308 katika kura za maoni nafasi ya ubunge viti maalumu , kushoto ni Samira Khalfan aliyepata kura 1,250.



Devotha Daniel Mshindi wa kwanza Uchaguzi wa UWT mkoa wa Kagera 
Devotha Daniel akipewa pongezi 



Na Mariam Kagenda , Kagera


Devotha Daniel Mburarugaba na Samira Khalfan Amour wameibuka washindi kati ya wagombea nane walioshiriki katika uchaguzi wa kura za maoni nafasi ya ubunge wa viti maalumu mkoa wa Kagera kupitia Umoja wa wanawake Tanzania (UWT).

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni mjumbe wa baraza ku
u UWT Taifa Yasmin Bachu amesema uchaguzi huo ulikuwa na wagombea nane, jumla ya wapiga kura walikuwa 1,483 ambapo kura moja ilihalibika hivyo kura halisi zilikuwa 1,482.

"Aliyeongoza kwa kura nyingi ni Devotha Daniel aliyepata kura 1,308 na wa pili Samira Khalfan aliyepata kura 1,250 wengine ni pamoja na Anitha Korongo kura 153, Elizabeth Ngaiza kura 94, Anitha Bunono kura 52, Anitha Nyamzinga kura 44, Herieth Lugaju kura 37 na Evastina Godian kura 26" amesema Bachu


Bachu amewashauri wajumbe wa UWT mkoa wa Kagera kuwa, wakati wa kampeini za Dk.Samia Suluhu Hassan wapaze sauti na kuunganisha nguvu za kumuombea kura zitoshe pia kushinda majimbo yote ya mkoa wa Kagera ili kuwawezesha washindi hao wawili kuingia bungeni.


Wagombea wamesema uchaguzi uliandaliwa kwa mazingira safi na Usalama wa hali ya juu na kuwaomba wenzao ambao kura hazikutosha kuendelea kuungana na waliochaguliwa kufanya kazi pamoja kwani wote ni wana chama wa chama cha Mapinduzi (CCM)


Devotha Daniel amewaomba wajumbe kuungana na kuondoa makundi kwani uchaguzi huo umepita wawe kitu kimoja wote walikuwa wazuri sasa wanajenga nyumba moja, hivyo itasaidia waweze kutafuta kura za Dk.Samia na majimbo yote nane kwa urahisi kwani ndilo jambo kubwa lililopo mbele yao kwasasa.

Mshindi mwingine Samira Khalfan ameshukuru kamati ya CCM Taifa kurudisha jina lake na kumuona anafaa katika nafasi hiyo, pia akawaasa wagombea wenzake ambao hawakufanikiwa kupata ushindi wasikate tamaa maana kwenye chama hicho zipo nafasi nyingi hivyo zinapotokea wasiache kugombea maana wote wanahitaji kutafuta kura usiku na mchana ili CCM ishinde.


Naye mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kagera Hajat Faidhah Kainamula amesema katika zoezi la kupata mgombea lipo suala la kupata na kukosa kuchaguliwa jambo la muhimu kwa sasa ni wajumbe kushikamana ili kuleta maendeleo mazuri ndani ya chama na siyo malumbano.

"Tuondoe chuki, baada ya uchaguzi kinachotakiwa katika chama ni mshikamano wenye kutenda,utekelezaji na kupata mafanikio mazuri yatakayoleta maendeleo" amesema Kainamula


Katibu wa UWT mkoa wa Kagera Rehema Zuberi amesema awali watia nia wa nafasi ya viti Maalumu walijitokeza wakiwa 13 mmoja kati ya hao hakurudilisha fomu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »