Waziri Ridhiwani Atoa Wito kwa Vijana Kuchangamkia Fursa Zilizopo

July 04, 2025
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo mikopo na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji Wananchi kiuchumi.

Mhe. Kikwete ametoa wito huo wakati alipotembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuuu lililopo katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa SABASABA, leo tarehe 04 Julai, 2025 Jijini Dar es Salaam.

“Serikali imeendelea kutenga fedha kuhakikisha makundi mbalimbali yananufaika, kwa mfano kupitia maelekezo ya kisera kwenye Sheria ya PPRA imeelekezwa asilimia 30 ya manunuzi yote ya umma ipelekwe katika kusaidia makundi ya Vijana, akinamama na Wenye Ulemavu," ameeleza Mhe. Ridhiwani.

Aidha, ameongeza kuwa upo mfuko maalumu wa kusaidia watu wenye ulemavu, lakini pia upo mfuko wa vijana na mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, hivyo mifuko yote hiyo kama vijana na wananchi wakiikimbilia hakika vilio vya uwezeshaji havitaweza kutokea.

Pia, Mhe. Kikwete amewata Waandishi wa Habari, Watumishi wa Umma na wadau mbalimbali kuzidi kupaza sauti juu ya uwepo wa mifuko hiyo na faida zake kwa wananchi .

Vilevile, ameelekeza Idara na Taasisi za serikali ziendelee kutoa elimu kwa wananchi hususani Vijana ili waweze kujua fursa za mikopo na uwezeshaji wananchi zilizopo.

“Maelekezo yetu ni kwamba Idara zetu zote, taasisi zetu zote waendelee kuhakikisha kwamba elimu inakuwa ndiyo kipaumbele kwa sababu serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mambo yaliyofanyika ni uwezeshaji wa kifedha, uwezeshaji wa watu, uwezeshaji wa kielimu, tumefanya mambo mengi sana na tumehakikisha watu wetu wanapatiwa elimu ili waweze kujinusuru katika maeneo haya” amebainisha Mhe. Ridhiwani.

Mbali na hayo Mhe. Ridhiwani amewataka Watanzania na hasa kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu kulinda amani iliyopo ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »