KAYA FOUNDATION YAKABIDHI VITI MWENDO, BIMA ZA AFYA KWA WATOTO WENYE ULEMAVU

February 14, 2026
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Taasisi isiyo ya kiserikali, Kaya Foundation, imekabidhi msaada wa viti mwendo vitano vilivyotolewa na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, pamoja na bima za afya kwa watoto wenye changamoto ya ulemavu, hatua inayolenga kupunguza vikwazo katika makuzi na elimu yao.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo Februari 14, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Kaya Foundation, Pili Ana Ngome, amesema taasisi hiyo imetoa viti mwendo vitano na kugharamia bima za afya kwa watoto 12 kupitia michango ya wananchi.

Amesema msaada huo unalenga kuwezesha watoto wenye ulemavu kuhudhuria shule kwa urahisi, akibainisha kuwa wengi wao wamekuwa wakikosa fursa ya elimu kutokana na ukosefu wa vifaa saidizi.

“Tumetoa msaada huu ili kuhakikisha watoto hawa wanapata haki yao ya msingi ya elimu. Viti mwendo vitawasaidia kufika shule na kushiriki kikamilifu katika masomo,” amesema.

Aidha, Ngome ametoa wito kwa jamii kujitokeza kuchangia ustawi wa watoto wenye ulemavu kwa kuwapatia bima za afya, akisisitiza kuwa uwekezaji huo utasaidia Taifa kupata wataalamu na wasomi wa baadaye.

“Lengo letu kuu ni kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu kama watoto wengine. Tusipowasaidia, Taifa litapoteza rasilimali watu muhimu,” ameongeza.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu wa Jiji la Dar es Salaam, Julieth Baingwa, ameipongeza Kaya Foundation kwa jitihada zake, akisema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia changamoto za watoto wenye ulemavu.

Naye mzazi wa mtoto aliyenufaika na msaada huo, Tatu Said Salum, ameishukuru taasisi hiyo akieleza kuwa kiti mwendo kitamwezesha mtoto wake kurejea shuleni.

“Mwanangu alishindwa kuendelea na masomo kwa kukosa kiti mwendo. Sasa ataweza kurudi shule na kuendelea na ndoto zake,” amesema.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »