Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akizungumza katika mkutano wa hadhara eneo la Kimani Mtaa wa Kinyamwezi, Kata ya Pugu, Ilala Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa ardhi Februari 13, 2026.
.....................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameamsha shangwe kwa wananchi baada ya kufanikiwa kumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu uliohusu eneo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya makaburi kudaiwa kuvamiwa na kujengwa nyumba za makazi ya watu.
Eneo linalodaiwa kuvamiwa lipo Kimani Mtaa wa Kinyamwezi, Kata ya Pugu, Ilala Jijini Dar es Salaam ambapo wakazi wa eneo hilo walimtuhumu Elizabeth Mwakapangala kuliuza huku akifukua makaburi bila ya kufuata sheria.
Mpogolo akizungumza na wananchi wa eneo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 13, 2026 ambao ulihudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya alisema eneo hilo lilitengwa na Serikali kwa ajili ya makaburi.
“Eneo hili lenye ramani ya upimaji namba E' 351\96, ya mwaka 2000, Kiwanja Na. 423 Kitalu N Pugu Mwakanga Kata ya Pugu Halmashauriya Jiji la Dar es Salaam lilitengwa kwa matumizi ya makaburi kwa mujibu wa mipango miji, lakini baadhi yetu yaani Mama Elizabeth alifungua kesi ya ardhi namba 202/2020 akiwa msimamizi wa mirathi ya Saidi Shomari Loko akiipeleka Halmashauri ya Jiji, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mahakamani,” alisema Mpogolo.
Mpogolo akisoma hukumu katika mkutano huo iliyotolewa na Mhe. Jaji A. M. Msafiri aliyesikiliza kesi hiyo ilielekeza mlalamikaji Bi Elizabeth alipwe fidia na siyo kuuza eneo la makaburi wala kufukua makaburi ya watu na kutupa mabaki ya miili hiyo dampo kama anavyodaiwa kufanya.
Aidha, Mhe. Jaji Msafiri alitoa muongozo mzuri kwa mlalamikaji wa namna ya kupata haki yake ya fidia na kueleza kuwa Mahakama haina mamlaka ya kufuta ramani ya mipango miji iliyoandaliwa na Serikali au kuhoji mamlaka ya Rais ya kutwaa ardhi kwa manufaa ya umma.
Mpogolo alisema kufuatia hukumu hiyo mlalamikaji hakuwa na haki ya kuuza eneo hilo wala kuhamisha makaburi na nikinyume na katazo la Sheria ya Mipango Miji katika Kifungu cha 3 (e) cha sheria hiyo.
Akisisitiza katika mkutano huo Mpogolo alisema uhamishaji wa makaburi upo kwa mujibu wa sheria za nchi na kueleza kuwa mtu yeyote hawezi akatoka na maamuzi ya kikao cha familia na kwenda kuhamisha mwili wa mtu aliyezikwa kwenye kaburi husika hata kama aliyezikwa ni baba au mama yake ni lazima afuate utaratibu uliopo kisheria na miiko ya dini zetu.
Alisema mlalamikaji Elizabeth anapaswa kufuata utaratibu wa kisheria ili pate haki yake na si vinginevyo.
Mpogolo alisema awali mlalamikaji alisimamishwa kufanya chochote kwenye eneo hilo analodai ni lake lakini hakufuata maelekezo na sasa Serikali imekata rufaa uamuzi wa Mahakama na kuhusu kufukua Makaburi na kutupa mabaki ya miili wanakwenda kushughulika naye kwa mujibu sheria.
Aidha Wananchi hao wamedai kuwa eneo lenye mgogoro lilitengwa kwa ajili ya maziko, kama walivyoelekezwa na serikali ya mtaa na watu waliohamishwa kutoka Kipawa kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amehudhuria mkutano huo kwa lengo la kuwasikiliza wananchi hao na kueleza wawe na amani na waendelee na shughuli zao ambazo zimepangiwa na serikali katika eneo hilo.
Bi. Elizabeth Mwakapangala amekanusha madai hayo akieleza kuwa hajawahi kufukua makaburi hayo na kwamba eneo hilo siyo eneo la Makaburi ni mali yake halali ambalo anazo nyaraka zote baada ya kushinda kesi mahakamani Oktoba 20, 2022.
![]() |
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, akizungumza wakati wa utatuzi wa mgogoro huo. |
Ukaguzi wa eneo lenye mgogoro ukiendelea
Ukaguzi wa eneo hilo ukiendeleaBicon zikiangaliwa eneo la tukio.Wananchi wakiwa kwenye eneo hilo.Msafara ukielekea kukagua eneo lenye mgogoroMkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo (kushoto), akioneshwa mipaka ya eneo hilo.Wananchi wakiwa eneo la lenye mgogoro.Wakina mama wakiwa eneo la mgogoro.











EmoticonEmoticon