MBUNGE WA TANGA MJINI AAGANA NA WAGENI KUTOKA QATAR NA OMAN

February 14, 2026

 MBUNGE WA TANGA MJINI AAGANA NA WAGENI KUTOKA QATAR NA OMAN WALIOKUJA KUJITOLEA  TANGA MJINI.

Mapema leo asubuhi, Mheshimiwa Kassimu Amari Mbaraka (Makbel), Mbunge wa Tanga Mjini, alikutana na kuagana rasmi na wageni wake kutoka Mataifa ya Qatar na Oman waliokuja Mkoani Tanga kwa dhamira ya kujitolea na kuchangia maendeleo ya kijamii.


Wageni hao walifika Jijini Tanga kwa ajili ya kushiriki katika ukarabati wa Shule ya Msingi Tongoni, pamoja na kutoa msaada wa vifaa vya malazi katika Shule ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum, hatua iliyopokelewa kwa furaha na shukrani kubwa kutoka kwa wananchi na uongozi wa Jiji la Tanga.

Katika mazungumzo yao ya kuagana yaliyofanyika ofisini kwa Mheshimiwa Mbunge, wageni hao walieleza kufurahishwa kwao na ukarimu mkubwa walioupata kutoka kwa wananchi wa Tanga pamoja na ushirikiano wa karibu kutoka kwa viongozi wa Jiji.


 Walisema wameguswa sana na mapokezi mazuri na mshikamano waliouona,  wakaahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Tanga.

Ikumbukwe kuwa wakati wa kampeni zake, Mheshimiwa Mbunge alisisitiza umuhimu wa kutumia fursa ya Diaspora kama chachu ya maendeleo ya Tanga.


Ujio wa wageni hao ni ishara ya utekelezaji wa maono hayo, yakionesha namna ushirikiano wa Kimataifa unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa jamii.


Kwa upande wake, Mheshimiwa Mbunge aliwashukuru sana wageni hao kwa moyo wao wa kujitolea na mchango wao mkubwa wa kijamii na kimaendeleo.


 Kama ishara ya kuthamini juhudi zao, aliwakabidhi vyeti vya shukrani kwa niaba ya wananchi wa Tanga Mjini.


*Imetolewa na Idara ya* *habari mawasiliano ofisi ya Mbunge*

*Tanga Mjini*

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »