SADC:SEKTA YA NISHATI IWE KICHOCHEO CHA KUIUNGANISHA AFRIKA KUJENGA UCHUMI

July 04, 2025


📌 *Yasisitiza utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ya Nishati*


📌 *Kapinga ataka SADC kuweka dhamira thabiti na mikakati madhubuti ya utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia*


Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Maji wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wametaka Sekta ya Nishati kuwa kichocheo cha kuiunganisha Afrika katika kujenga uchumi wake.


Wamesema hayo leo Julai 4, 2025  wakati wakihitimisha mkutano wa SADC jijini Harare nchini Zimbabwe ambao ulilenga kuimarisha na kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha mtangamano wa Kikanda katika sekta za nishati na maji.

Akizungumza wakati akihitimisha mkutano huo, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Umeme wa Zimbabwe, Mhe. Dkt. July Moyo, ameitaka jumuiya hiyo ya SADC kuipa kipaumbele sekta ya nishati na maji ili kuifanya kuwa na tija kwa wananchi katika kukuza uchumi wao kwa kuwa nishati  ni chanzo kikubwa cha maendeleo. 

Aidha, ameipongeza Tanzania kwa kuandaa na kuwa mwenyeji wa kufanikisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Nishati Afrika wa Misheni 300 (M300) ambao ulifanyika kwa mafanikio. Pia, Dkt. Moyo amezishukuru Nchi wanachama zilizohudhuria katika mkutano huo muhimu uliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Malawi, Mhe. Ibrahim Matola ameitaka SADC kuhakikisha inaiendeleza miradi yote ya kipaumbele katika jumuiya ili kuifanya sekta ya nishati kuwa kimbilio katika kujenga uchumi wa nchi zao. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameitaka SADC kuhakikisha inakuwa na mikakati madhubuti ya utekekezaji wa maazimio mbalimbali wanayofikia  katika makongamano ya umoja huo ili yawe na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla na kuifanya sekta ya nishati kuwa chachu na mkombozi ndani ya SADC. 

Kuhusu utekelezaji wa nishati safi ya kupikia katika jumuiya hiyo, Mhe. Kapinga ameitaka SADC kuweka dhamira thabiti na mikakati madhubuti ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia ili kuwafikia watu wengi zaidi katika SADC. 


Mkutano huo uliohitimishwa leo, umehudhuliwa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Suzan Kaganda, Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Mha. Styden Rwebangila, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy, Mkurugenzi wa  Mipango na Uwekezaji (TPDC), Derick Moshi, Mkurugenzi wa Mifumo ya Udhibiti Umeme (TANESCO) , Mha. Deogratius Mariwa, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi (EWURA), Msafiri Mtepa na  Wataalam kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »