OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI NA CLYDE &CO AFRIKA KUSHIRIKIANA KUWANOA MAWAKILI

July 29, 2025
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka kampuni ya Kimataifa ya uwakili ya Clyde & Co Afrika kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kufungua fursa ya mafunzo kwa Mawakili wa Serikali.

Naibu Mwanasheria Mkuu amekutana na ujumbe huo tarehe 25 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba Jijini, Dodoma.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kushirikiana na Taasisi hiyo kwenye eneo la mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kurahisishia utendaji kazi.

Aidha, amesema kuwa wanatarajia taasisi hiyo kutoa mafunzo na ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya Sheria ikiwa ni pamoja na masuala ya Usuluhishi wa migogoro ya kimataifa, Sheria za mikataba ya kimataifa na masoko ya mitaji, sheria za Biashara na uwekezaji, Sheria za Miradi na Ujenzi, Sheria za Miundombinu, Sheria zinazosimamia Bandari, Viwanja vya Ndege na Reli, Masuala ya Nishati, Sheria za Madini, Sheria za mabenki na taasisi za Fedha, Akili mnemba/unde, usimamizi wa mikataba/miradi, maktaba mtandao (e-library) pamoja na fursa za kushikishwa (attachment).

“Tuko tayari kushirikiana nanyi katika maeneo haya ya mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Clyde & Co Afrika Bw. Peter Kasanda ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha na mafunzo kwenye masuala yote ambayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapendelea kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali.

“Sisi tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Ofisi hii kubwa ya kisheria, amesema kuwa kampuni yake iko tayari kushirikiana nanyi katika masuala ya mafunzo ili kuweza kuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »