Na Mwandishi Wetu, JAB.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, (Journalists Accreditation Board-JAB) imetakiwa kuhakikisha kuwa, waandishi wa habari wote nchini wanazingatia sheria, kanuni, viwango vya juu vya weledi, maadili, uwajibikaji, na miongozo inayosimamia taaluma ya uandishi wa habari.
Maelekezo hayo ni kati ya maagizo saba yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (MB), katika hotuba yake ya uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika tqrehe 03 Machi, 2025, katika Ukumbi wa Hotel ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Profesa Kabudi amesema, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari itasaidia kudhibiti uandishi usio wa kimaadili na kuongeza heshima ya taaluma hiyo, hivyo inatakiwa kuanza kwa kuwalea na kuwapa miongozo mbalimbali kuhusu taaluma yao.
Profesa Kabudi ameitaka pia Bodi hiyo kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma kwa kutoa miongozo ya mafunzo ya mara kwa mara, na kuwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko na ukiukwaji wamaadili kwa haki na uwazi.
Agizo la pili kwa Bodi ni kuandaa na kusimamia utaratibu wa usajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma, huku akisisitiza kuwa mfumo huo unatakiwa kua shirikishi na wenye kuendana na maendeleo ya teknolojia na mazingira ya sasa ya sekta ya habari.
Ameitaka JAB kuhakikisha inashirikiana na vyombo vya habari, vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari, na wadau wengine ili kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mafunzo ya mara kwa mara na kuwa na ujuzi wa kisasa.
Profesa Kabudi ameiagiza Bodi kuandaa programu za uelimishaji ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa taaluma ya uandishi kusimamiwa ipasavyo.
Amesisitiza kuwa ni muhimu Bodi pia ikasaidia kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanatumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili, katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali, ikiwemo kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika utoaji wa habari.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi Bodi inapaswa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa usalama bila vitisho, unyanyasaji, au vikwazo visivyo vya lazima, kwani Usalama wa wanahabari ni msingi wa uhuru wa vyombo vya habari.
Akitangaza kuzinduliwa rasmi kwa Bodi hiyo, Profesa Kabudi amesema, Serikali inatambua umuhimu wake, katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na kuahidi kuwa itaendelea kushirikiana nayo ili kuhakikisha taaluma ya habari inaimarika kwa manufaa ya taifa.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 ya Sheria za Tanzania, ipo chini ya Mwenyekiti Mzee Tido Mhando.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula, amewataka waandishi wa Habari kuilinda taaluma ya uandishi wa Habari kwa kuwa hakuna atakayeilinda zaidi ya wao wenyewe.
EmoticonEmoticon