Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (kulia) akizindua rasmi Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (Journalists Accreditation Board-JAB) na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando (kulia) leo Machi 3, 2025 jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) amesema, kuwathibitisha (accredit) waandishi wa habari ni hatua muhimu katika kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inazingatia viwango vya kitaaluma, maadili, na uwajibikaji.

"Kupitia ithibati, itaonyesha waandishi wa habari wenye sifa stahiki na waliopata mafunzo yanayohitajika ili kufanya kazi kwa ufanisi" amesema Profesa Kabudi na kuongeza kuwa, "Hii itasaidia kuimarisha weledi katika tasnia ya habari na kudhibiti usambazaji wa habari zisizo sahihi".
Amesema, vile vile, ithibati itasaidia kulinda haki na uhuru wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, kwani waandishi wa habari wanaotambulika rasmi wana nafasi nzuri ya kulindwa dhidi ya vitisho, manyanyaso, na madhila wanayoweza kukutana nayo wakiwa kazini.
Profesa Kabudi amesema, katika dunia ya sasa yenye wingi wa habari kupitia mitandao ya kijamii, ithibati ni njia bora ya kudhibiti usambazaji wa habari za uongo (fake news), hivyo kupitia utambulisho rasmi wa waandishi wa habari, wananchi wanaweza kutambua vyanzo vya kuaminika vya habari na kuepuka upotoshaji unaoweza kuleta taharuki katika jamii.
Amesema, ithibati pia itachochea uwajibikaji kwani waandishi wa habari walioithibitishwa wanawajibika kwa Bodi, jambo litalorahisisha usimamizi wa maadili ya taaluma ya habari.
"Ikiwa mwandishi wa habari atakiuka maadili ya uandishi wa habari, ni rahisi kuwajibishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, hivyo itasaidia kudumisha weledi na uwajibikaji katika sekta ya habari," amesisitiza Prof. Kabudi.
Amesema, kuthibitishwa au kupewa Ithibati na Bodi kunakuza hadhi na heshima ya taaluma ya uandishi wa habari, kama ilivyo kwa taaluma nyingine kama sheria na udaktari.
"Uandishi wa habari hauna budi kutambuliwa rasmi kama taaluma yenye hadhi na umuhimu mkubwa katika jamii" amesema Profesa Kabudi.
Amesema, kupitia ithibati, waandishi wa habari wanapata utambulisho rasmi unaowawezesha kufanya kazi zao kwa uadilifu, na pia itawarahisishia kupata habari kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Gerson Msigwa, amesema Bodi ya Ithibati chini ya Wizara hiyo, itakuwa na jukumu la kusimamia maadili ya taaluma na kusaidia kukuza mazingira bora ya utendaji kazi katika Sekta ya Habari hapa nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo, Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekazia kuwa Bodi hiyo itawajibika kuhimiza waandishi wa Habari kuandika kwa weledi, na kuzingatia ukweli, haki na maslahi ya umma.
Amebainisha kuwa Bodi ya Ithibati yenye wajumbe 7 akiwemo Mwenyekiti wake Tido Mhando, itashirikiana na Taasisis za mafunzo na wadau mbalimbali wa tasnia ya Habari kuhakikisha waandishi wa Habari wanapata elimu bora na mafunzo yanayokidhi viwango vya kitaaluma.
Akitoa shukurani zake Mhando amemhakikishia Waziri Kabudi kuwa wajumbe wa Bodi hiyo wamepokea maelekezo aliyowapa na kwamba watayatekeleza kwa moyo wa uzalendo, uadilifu na ufanisi wa hali ya juu kwa ushirikiano na wadau wa sekta ya Habari.
Amesema kwa kuonyesha utayari wa kufanya kazi, vikao vya Bodi ya ithibati vitaanza Jumanne Machi 4;2025, kwa lengo la kupanga mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo yaliyoainishwa kwa mujibu wa sheria.
EmoticonEmoticon