TANZANIA YAVUNJA REKODI ONGEZEKO LA WANYAMAPORI

March 03, 2025


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema ongezeko la idadi ya Wanyamapori katika hifadhi za Wanyama hapa nchini imetokana na juhudi za serikali kushirikisha wadau wa uhifadhi wa Wanyamapori na wananchi kwa ujumla hali iliyopelekea kukua kwa utalii na uchumi katika Taifa.



Ameyasema hayo leo Machi 03, 2025 jijini Dodoma katika maadhimisho ya 11 ya  Siku ya Wanyamapori Duniani ambapo amesisitiza Tanzania inaongoza Duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama aina ya Simba, Chui, Nyati na ni ya tatu kwa idadi wa Tembo Duniani huku akifafanua kuwa mafanikio hayo ni kutokana na kuitangaza vyema sera ya Utalii ndani na nje ya nchi na kuboresha jeshi la uhifadhi.


“Wanyamapori ni rasilimali muhimu katika uchumi wa nchi yetu kupitia utalii ambao unachangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni, asilimia 17.1 ya Pato la Taifa na ajira takribani milioni 1.6 zilizo rasmi na zisizo rasmi, hadi Mwaka 2024, Sekta ya Utalii imevunja rekodi kwa kufikia jumla ya watalii 5,360,247 na watalii wa Kimataifa imefikia 2,141,895 huku watalii wa ndani wakiwa 3,218,352. Kutokana na mapato ya utalii imefikia  Dola za Marekani Bilioni 3.9” Amesema Waziri Chana 

Aidha, ameweka bayana kuwa juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii kwa vitendo ndani na nje ya nchi kupitia Programu ya Tanzania the Royal Tour na Amazing Tanzania imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza hamasa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea hifadhi za utalii na Wanyamapori hapa nchini

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Chana amesema Serikali kupitia Wizara Hiyo imeendelea kushirikiana na wadau wa uhifadhi kuchukua jitihada za makusudi ikiwemo kulinda na kuendeleza uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, kudhibiti ujangili wa nyara na kitoweo na uhifadhi endelevu wa mapito ya wanyamapori ili kuimarisha mifumo ikolojia ya uhifadhi sambamba na ushirikishwaji wa jamii kupitia maeneo ya Jumiya za Hifadhi za Wanyamapori.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Maliasili, CP. Benedict Wakulyamba amesema Wizara itaendelea na mikakati ya kutunza na kuhifadhi Wanyamapori kwa kuweka mazingira wezeshi na kutangaza sera ya Utalii nje ya nchi kwa kukaribisha wawekezaji, kuboresha maeneo ya hifadhi, kuboresha maisha kwa watumishi na wahifadhi na vitendea kazi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara  ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alexander Lobora amesema   lengo la siku hiyo ni kuhamasisha Jamii juu ya Uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na mimea iliyohatarini kutoweka, kupunguza uharibifu wa mazingira na kupinga ujangili.


"Siku hii adhimu inatoa fursa ya kutoa na kuonesha mchango kwa wahifadhi wa Wanyamapori na Wantama katika maisha ya bai anoai na hatua za kulinda Wanyamapori kwa manufaa ya Taifa kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho" amesema Dkt. Lobora.



Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni "Wanyamapori na Uwekezaji Kifedha, Wekaza kwa watu na Dunia" inalenga  kuhimiza  mfumo na mikakati endelevu ya kusimamia na kutumia rasilimali fedha katika hifadhi wa rasilimali za Wanyamapori na nyara zake

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »