📌 Tanzania na Oman kufungua fursa mpya za ushirikiano
📌 Dkt. Biteko atoa wito nchi za Afrika ziruhusiwe kutumia rasilimali zake kuzalisha umeme
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Oman ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 44 ni wa kihistoria na umeendelea kuwa na manufaa baina ya nchi hizo mbili.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Februari 28, 2025 ofisini kwake Jijini Dar es salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud Hilal Al Shidhani.
“ Mhe. Balozi tunakushukuru kwa namna tunavyoshirikiana na uwepo wako nchini umeendelea kuimarisha mahusiano na Serikali yako. Tunafurahia kuwa na uhusiano huu wa kidiplomasia. Sisi tunaichukulia Oman kama marafiki na Mhe. Rais Samia anapenda ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zingine, kanuni inayosema ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako ni muhimu sana, amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kusema kuwa uwepo wa idadi kubwa ya Watanzania wanaofanya kazi nchini Oman ni tafsiri ya urafiki na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo.
Dkt. Biteko amesema kuwa Tanzania itapeleka timu ya wataalamu nchini humo ili kujifunza kuhusu masuala ya gesi. Pia, amemweleza Mhe. Balozi Al Shidhani kuhusu nia ya Serikali ya kufanya mnada wa tano wa vitalu vya gesi kupitia Kongamano la Mkutano wa 11 wa Afrika Mashariki wa Petroli kuanzia Machi 5 - 7 mwaka huu, hivyo mnada huo ni fursa kwa kampuni za kutoka nchini Oman kuwekeza nchini.
Aidha, fursa zingine zinazotokana na ushirikiano huo ni kuendeleza ufadhili wa masomo kwa vijana wa Tanzania kwa ajili ya kusoma nchini Oman hususan katika masuala ya biashara, mafuta na gesi.
“ Ushirikiano wetu wa Wizara ya Nishati na Serikali ya Oman haukwepeki katika mnyororo mzima kuanzia uzalishaji hadi katika biashara. Tupo kwenye njia sahihi na tunaamini katika ushirikiano huu tutapiga hatua zaidi na tutaacha alama,” amesema Dkt. Biteko
Akizungumzia kuhusu ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia amesema kuwa nchi za Afrika na nchi zinazoendelea zizungumze lugha moja kuhusu namna ya kuzalisha nishati kwa ajili ya kusaidia watu milioni 600 wanaokosa nishati Barani Afrika kwa kutumia rasilimali zilizopo huku akitolea mfano baadhi ya nchi zilizondelea kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha umeme lakini kutoruhusu nchi za Afrika kufanya hivyo.
“ Afrika hatufanyi uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa kama nchi zilizoendelea na pia kama kuna teknolojia wanayoweza kutupa basi itumike ili kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa, lakini kiwango cha uchafuzi hakifanani kati ya nchi hizi hivyo masharti kuhusu kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa hayapaswi kuwa sawa kwa wote. Hivyo tunahitaji kuzungumza lugha moja na nimeona baadhi ya nchi za Bara la Asia zinazungumza lugha moja katika hili,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Pia, amezipongeza Kampuni za nchini Oman zinazofanya biashara Tanzania kwa kuendelea kufanya shughuli zao kwa ufanisi pamoja na kuzikaribisha kuwekeza katika sekta ya gesi kwa kuwa nchi ina kiwango kikubwa cha gesi baada ya kuhamia katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji.
Kwa upande wake, Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud Hilal Al Shidhani amesema kuwa nchi yake inafurahia uhusiano uliopo kati yake na Tanzania na wanajivunia kuwa na watu zaidi ya asilimia 30 wanazungumza lugha ya Kiswahili kati ya watu milioni 9 waliopo nchini humo.
Balozi Shidhani amesema kuwa nchi yake ina uelewa mkubwa zaidi kuhusu masuala ya mafuta na gesi hivyo inaweza kuisaidia Tanzania kwa kuwajengea uwezo wataalamu wake, halikadhalika Tanzania inaweza kuisaidia nchi yake katika masuala ya madini kwa kuwa imepiga hatua zaidi katika eneo hilo.
“ Kuna maeneo mengi tunayoweza kushirikiana na Tanzania mfano hapa kuna umeme wa ziada na sisi hivi karibuni tumefungua kituo cha kuzalisha hydrojeni na Tanzania inaelekea huko hivyo kama kuna fursa mpya tunaweza kushirikiana kwa karibu,” amesema Balozi Shidhani.
Ameongeza kuwa nchi yake imeandaa jukwaa maalum kwa ajili ya kutoa fursa za ufadhili wa masomo kwa Watanzania, pia ameahidi kuwa nchi yake itachimba visima vya maji 20.
EmoticonEmoticon