RAIS SAMIA :NATAMANI TANGA IWE KITUO KIKUBWA CHA UTALII

February 28, 2025


Na Happiness Shayo-Tanga


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanga inaweza kuwa kivutio na kituo kikubwa cha utalii kutokana na jiografia  yake.


Ameyasema hayo leo jijini Tanga katika uwanja wa Mkwakwani alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa huo.

"Naitamani Tanga ambayo itakuwa na utalii wa fukwe, historia na utamaduni. Tanga hii kwa maumbile yake ni kivutio tosha cha utalii kwa fukwe zake, milima, miinuko yake lakini pia utajiri wake wa kihistoria kwa kuzingatia hulka na ukarimu wa watu wake,pia kwa sababu kuna mapango ya Amboni, Magofu ya Pangani, Misikiti ya Kale,watu mashuhuri kama Shaban Robert na Utalii wa Kiutamaduni‘’alisema Rais Samia.

Rais Samia amesisitiza kuwa ili ndoto ya kuwa kituo cha Utalii itimie ni lazima watu wa Tanga wawe tayari kuifanyia kazi ndoto hiyo kwa kuendelea kuwa kitu kimoja baina ya Chama na Serikali na kuzungumza lugha moja.


Aidha, Rais Samia amewataka wananchi hao kuchangamkia fursa zitokanazo na ndoto hiyo, akitolea mfano wa uwepo wa Bandari wenye fursa mbalimbali ikiwemo uwakala wa forodha.

 "Jifunzeni taratibu na vigezo vya kuwa wakala wa forodha bandarini ili mnufaike. Haipendezi tunatanua fursa za kiuchumi watu wa mikoa mingine waje wafaidike na fursa hizo, hivyo Tanga jipangeni vizuri" Rais Samia amesisitiza. 


Kwa upande wa taaluma ya utalii, Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Tanga kujifunza  taaluma zinazohusiana na Utalii hasa kupitia vyuo mbalimbali vilivyoko Mkoani hapo akitolea mfano wa Chuo cha Amani.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »