WAZIRI KABUDI KUZINDUA BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI MACHI 3

February 28, 2025

 

Na Mwandishi Wetu, JAB, Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Palamagamba Kabudi, Wiki ijayo anatarajiwa kuzindua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB). 

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa imeeleza kuwa uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 03 Machi, 2025 katika Hotel ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam. 

Katika Uzinduzi huo Waziri Kabudi pia atamkabidhi zana za Kazi Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Tido Mhando, zinazojumuisha Sera ya Habari, Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni zake. 

Miongoni mwa majukumu ya Bodi hiyo yanayotarajiwa kuanza kutekelezwa mapema mara baada ya kuzinduliwa ni pamoja na kutoa Ithibati na Vitambulisho (Press Card) kwa Waandishi wa Habari waliokidhi vigezo vilivyoainishwa kisheria na kusimamia maadili ya taaluma ya Uandishi wa Habari. 

Kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imepewa mamlaka ya kutoa Vitambulisho kwa Waandishi wote kutoka vyombo vya habari vya umma, binafsi, pamoja na waandishi wa kujitegemea. 

Awali, utoaji wa vitambulisho hivyo kwa Waandishi wa Habari ulikuwa ukifanywa na Idara ya Habari-MAELEZO kabla Bodi ya Ithibati kuundwa na kuanza majukumu yake rasmi. 

Bodi hiyo ilitangazwa Septemba 18 mwaka jana baada ya Waziri mwenye dhamana kumteua Bw. Mhando na wajumbe wengine sita kuunda bodi hiyo, sanjari na kuwahamishia watumishi sita kutoka wizarani kuunda Sekretarieti ya bodi hiyo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »