RAIS SAMIA ASIFU MAFANIKIO YA PROGRAMU YA MWANAMKE KIONGOZI

February 21, 2025

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia Programu ya Mwanamke Kiongozi (Female Future Program) katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.


Akizungumza katika hafla ya mahafali ya awamu ya 10 ya programu hiyo iliyoandaliwa na Chama cha waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika katika ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesisitiza kuwa uwekezaji katika uongozi wa wanawake ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

“Programu hii imeonesha kuwa wanawake wakipewa nafasi na mafunzo sahihi, wanaweza kushika nafasi za juu za uongozi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii,” amesema Rais Samia huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza jitihada hizo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran, amemshukuru Rais Samia kwa kuwa sehemu ya safari hiyo tangu alipoizindua mwaka 2016 akiwa Makamu wa Rais.

Ndomba-Doran ameeleza kuwa programu hiyo imewanufaisha wanawake 642, ikiwa ni pamoja na wabunge 150 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

"Katika kipindi cha miaka 10, wanawake 102 waliopitia mafunzo haya wamepanda kwenye ngazi za juu za uongozi, huku wengine 50 wakichaguliwa kuwa wajumbe wa bodi mbalimbali na sita wakiongoza taasisi tofauti. Pia, Jeshi la Polisi limeonesha nia ya kushiriki programu hii kwa maafisa wake wa kike, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika vyombo vya usalama". Amesema Ndomba

Amesema, Ili kuimarisha mtandao wa wanawake viongozi, ATE imeanzisha Female Future Tanzania Network, jukwaa litakalowezesha wahitimu wa programu hiyo kuendelea kushirikiana na kusaidiana katika safari zao za uongozi.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi kutoka serikali, sekta binafsi, mabalozi, na wadau mbalimbali wa maendeleo. Wahitimu wa awamu ya 10 walipokea vyeti vyao huku wakihamasishwa kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika uongozi wa wanawake Tanzania.

Bi. Ndomba-Doran alihitimisha kwa kutoa shukrani kwa wadhamini na washirika wa programu hiyo, akisisitiza kuwa uwekezaji katika wanawake ni uwek
ezaji katika maendeleo ya taifa.






Share this

Related Posts

Previous
Next Post »