RAIS SAMIA ATOA BILIONI 16.696 KWA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU MKOANI TANGA KUPITIA MRADI WA SEQUIP.

July 09, 2025
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, imetoa jumla ya shilingi bilioni 16.696 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) mkoani Tanga.

Kati ya fedha hizo, jumla ya shilingi bilioni 4.450 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga, ambayo tayari imekamilika. Miundombinu hiyo ni pamoja na madarasa 22, maabara, mabweni 12, bwalo la chakula, jengo la utawala na nyumba tano za walimu.

Akizungumza Kaimu Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Tanga, Mwalimu Joel Laizer, amesema kuwa serikali pia imetoa shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Mkoa ya Amali katika Wilaya ya Mkinga, ambapo ujenzi unaendelea kwa kasi.

Aidha, serikali imetoa shilingi bilioni 5.842 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 10 za SEQUIP katika halmashauri tisa za Mkoa wa Tanga. Vilevile, kiasi cha bilioni 3.505 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule sita za Amali katika halmashauri tano, ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa upande mwingine, jumla ya shilingi bilioni 1.274 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 13 za walimu, ambazo kwa sasa zipo katika hatua ya ukamilishaji.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga, Mwalimu Chuki Athumani, pamoja na Mwalimu wa TEHAMA, Obed Mndota, wameipongeza serikali kwa kazi kubwa ya kujenga shule hiyo kwa kiwango na ubora wa hali ya juu, ikiwa na miundombinu yote muhimu ya kitaaluma na kijamii.

Wanafunzi Anjela Cosmas na Jessica Mussa nao wametoa pongezi kwa Serikali kwa kumthamini mtoto wa kike kwa kuhakikisha wanajengewa mazingira bora ya kujifunza. Wamesema kuwa ndoto zao sasa zinaonekana kutimia kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu shuleni.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Parungukasera kilichopo Wilaya ya Mkinga, Bi. Neema Mashimba, amesema kuwa ujenzi wa shule ya Amali kwa kiasi cha bilioni 1.6 unaendelea kwa kasi na kukamilika kwake kutasaidia kuongeza ufanisi wa elimu na ujuzi kwa watoto wengi wa eneo hilo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »