📌 *Ni uliosaoniwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Misheni 300*
📌 *Unalenga kufikisha umeme kwa wananchi milioni 8.3 ifikapo 2030*
📌 *Unaelekeza asilimia 75 ya wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2030*
📌 *Katibu Mkuu Nishati asema sasa ni muda wa utekelezaji*
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameongoza kikao cha Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake ambacho kimelenga kujadili utekelezaji wa Mpango Mahsusi wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact) ambao ulisainiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Misheni 300 mwezi Januari 2025 ukilenga kuunganishia umeme wananchi milioni 8.3 ifkapo 2030 na kufikisha Nishati Safi ya Kupikia kwa asilimia 75 ya Watanzania.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu.
“Baada ya Mpango huu Mahsusi wa Nishati kusainiwa, kinachofuta ni utekelezaji, hivyo kufanyika kwa kikao hiki itatuwezesha kufahamu tunapoelekea, miradi tuliyopanga kutekelezwa itatekelezwaje, fedha zinapatikanaje, sekta binafsi zinashirikishwaje na je kuna sera, kanuni na sheria zozote tunazopaswa kubadilisha ili kuendana na mpango huu, hivyo lazima tuwe na majibu ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi mpango huu.” Amesema Mhandisi Mramba
Mhandisi Mramba amesema kuwa, mpango huo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa kutosha ili kuweza kuufikisha kwa wananchi, viwanda, taasisi zinazotoa huduma za kijamii n.k hivyo aliwaelekeza Watendaji wa Wizara na Taasisi kuhakikisha kuwa miradi inayopaswa kutekelezwa inaainishwa ipasavyo ili kuweza kupata fedha za kutekelezaji miradi hiyo.
“ Kwa sasa tuna umeme wa kutosha lakini hatuwezi kubweteka na umeme uliopo sababu mahitaji yanazidi kuongezeka ikiwemo viwanda, treni za umeme na migodi ambayo inatumia umeme mkubwa, ni lazima tuiweke mipango yetu vizuri ili tuweze kupata fedha za kutekeleza miradi mipya na hili linawezekana kwa sababu Mpango wetu Mahsusi ndio ulionekana kuwa bora kuliko ya nchi nyingine za Afrika. “Amesisitiza Mramba
Mhandisi Mramba aliongeza kuwa, ili kufikia malengo ya Mpango huo ni lazima sasa Wizara na Taasisi zake ziache kufanya kazi kwa mazoea. Utaratibu wa kufanya kazi lazima ubadilike ambapo TANESCO na REA zimetakiwa kuwa wabunifu na kuja na utaratibu tofauti ya kufanya kazi ili kufikisha lengo la kuunganisha wateja milioni 1.7 kwa mwaka kutoka wateja 500,000 wa sasa.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).
EmoticonEmoticon