WAENDELEZAJI TEKNOLOJIA ZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA WASISITIZWA KUONGEZA UBUNIFU

July 10, 2025
-Lengo kila Mtanzania amudu gharama

-Watakiwa kutanua wigo wa usambazaji wa bidhaa

Waendelezaji wa Teknolojia za Nishati Safi ya Kupikia watakiwa kubuni bidhaa ambazo kila mwananchi anaweza kumudu gharama zake sambamba na kuhakikisha wanatanua wigo wa upatikanaji wa bidhaa hizo kote nchini.

Rai hiyo imetolewa Julai 10, 2025 na Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mha. Ahmed Chinemba alipotembelea Banda la REA na kuzungumza na waendelezaji na wasambazaji wa teknolojia na bidhaa za nishati safi ya kupikia waliopo katika banda hilo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.

"Tunavyoandaa na kusambaza bidhaa za nishati safi ya kupikia ni vyema tukaongeza ubunifu ili kuhakikisha kila mwananchi wa kipato chochote kile anamudu gharama," alisisitiza Mha. Chinemba.

Mbali na suala la ubunifu, Mhandisi Chinemba aliwasisitiza kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa endelevu ili kuepuka kutoa mwanya wa kuhama kwa mwananchi ambaye tayari ameanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Alisema waendelezaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia hususan watengenezaji wa mkaa mbadala wanapaswa kuwa na bidhaa za kutosha ili kila zinapohitajika zinapatikana

"Hatupaswi kumpa sababu mwananchi ambaye tayari anatumia nishati safi ya kupikia kurudi kwenye matumizi ya nishati zisizo salama, mhakikishe mnakuwa na uzalishaji unaojitosheleza; bidhaa zinapaswa kuwepo muda wote ili mwananchi anavyoishiwa anapata kwa urahisi," alielekeza.

Aliwasisitiza kuhakikisha wanapanua wigo wa usambazaji ili kila kona ya nchi bidhaa hizo za nishati safi ziwe zimefika na kumuwezesha mwananchi kuwa na chaguo kulingana na kipato chake.

Mhandisi Chinemba alielekeza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu ili kuwaondolea wananchi dhana potofu ya kwamba kutumia nishati safi ya kupikia ni gharama kuliko kutumia nishati zingine zilizozoeleweka.

"Tuendelee kutoa elimu na kuhamasisha wananchi maana kama ni umeme sasa hivi kila kijiji kinao ni wakati sasa wa kumhamasisha mwananchi aishie kijijini kutumia umeme kwa matumizi mengine pia mbali na kuwasha taa," alisisitiza Mha. Chinemba.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »