Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia na kutenga shilingi bilioni 28.1 kwa ajili ya kutekeleza Kampeni Kabambe ya Utoaji wa chanjo ya Mifugo Kitaifa ili kudhibiti na kutokomeza magonjwa yakipaumbele nchini.
Hayo yamefahamika wakati Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alipomwakilisha Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la 42 la Chama Cha Madaktari wa Wanyama kwa mwaka 2024 linalofanyika jijini Arusha Disemba 3, 2024.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mhe. Rais Samia, Waziri Ulega amesema kuwa kampeni hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi Januari 2025 imelenga kudhibiti na kutokomeza magonjwa ambayo ni vikwazo dhidi ya biashara ya mifugo na mazao yake kimataifa.
Amebainisha kuwa chanjo kwa mifugo itasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo, kuongeza kiwango cha uuzaji wa mazao ya mifugo nje ya nchi, kukuza pato la fedha za kigeni nchini.
Ameongeza kuwa chanjo pia itasaidia kuimarisha afya ya jamii kwa kuzuia matumizi makubwa ya dawa za antibayotiki kwa wanyama na kuzuia magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Halikadhalika, amefafanua kuwa programu hiyo inatarajiwa kutoa ajira za muda mfupi kwa vijana 3,540 ambao ni wataalam wa afya ya mifugo walioko nje ya ajira rasmi katika mikoa yote.
Aidha, kupitia programu hiyo ya miaka mitano (5) jumla ya ng’ombe 19,097,223 watachanjwa dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ngo’mbe, mbuzi na kondoo 20,900,000 watachanjwa dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo.
Vilevile kupitia programu hiyo jumla ya kuku wa asili 40,000,000 watachanjwa dhidi ya ugonjwa wa kideri/mdondo ili kupunguzavifo na kuongeza uzalishaji, kuimarisha lishe ya jamii na kipato kwa kaya.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ametumia jukwaa hilo kutoa rai kwa madaktari wa wanyama na madaktari wasaidizi kuwa mstari wa mbele kutelekeza majukumu yao pale zoezi hilo itakapozinduliwa mapema mwezi Januari 2025.
EmoticonEmoticon