RC TANGA ATOA MAAGIZO KWA RUWASA KUSIMAMIA UANZISHWAJI WA VITALU VYA MITI

November 01, 2024

 

Na Denis Chambi, Tanga.

MKUU wa mkoa wa Tanga  Balozi Dkt. Batilda Buriani  ameuwagiza Wakala wa Maji vijijini 'RUWASA' kuhakikisha wanasimamia jumuia zote za watumia Maji ziweze kuanzisha vitalu vya miti ambayo itapandwa karibu na vyanzo vya Maji ili kuweza kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mji wakati wote.

Dkt Buriani ametoa maelekezo hayo wakati wa ya  hafla kukabidhi  gari lenye thamani ya shilingi Million 154 pamoja na pikipiki mbili zilizotolewa na wizara ya maji ambazo zimegharimu kiasi cha shilingi Million 4 ambazo zitakwenda kutumiwa na watumishi wa RUWASA katika Wilaya za Pangani na Korogwe kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao sambamba na kuendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

"Kama tunavyojua sera ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndio kichwani, vyombo hivi vinakwenda kuendelea kuhakikisha hakuna changamoto ya upatikanaji wa maji  na kufikia adhima ya Serikali ya kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini ifikapo 2025" 

"Lakini pia wizara imetuletea pikipiki mbili  zinazokwenda kwa vyombo vya jumuiya za watumiaji wa maji 'CBWSO' za Mkombozi wilayani Pangani  na Mwakipokwa iliyoko  Korogwe kwaajili ya kwenda kuboresha upatikanaji wa maji katika vijiji vyetu"

"Tumekubaliana kwamba Tanga ya kijani inawezekana  tumeanza mikakati mahususi ya kuendelea kutumia wadau wetu wote kupanda miti tukitumia utaalam wa wenzetu wa  Wakala wa Misitu Tanzania 'TFS' ili tuweze  kupanda miti sahihi kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukipanda miti ambayo inakindhana na  hali ya hewa tunataka  miti ambayo itasaidia mazingira" 

"Tumekubaliana na viongozi wa jumuiya za watumika Maji na tumesisitiza miche iwe karibu na Wananchi ili tukianzisha zoezi la upandaji wa miti  tuweze kupanda kwa pamoja  meneja wa mkoa ulisimamie hilo  ili ionekane kwamba kweli hili ambalo tumekubaliana kwenye mikutano liweze kutimia" alisisitiza Dkt. Buriani.

Meneja wa Wakala wa Maji vijijini 'RUWASA' mkoa wa Tanga Mhandisi  Upendo Lugongo amesema kuwa kupatikana kwa vyombo hivyo vya usafiri kwa Wilaya za Pangani na Korogwe  kunawapa motisha ya utendaji kazi  watumishi ambao wanapambana kuhakikisha huduma ya maji kwa wananchi inaimarika.

"Pikipiki hizi pamoja na gari hili vinakwenda kuboresha utoaji huduma kwa wananchi kuwafikia kule waliko  lakini kikubwa zaidi mazingira ya utendaji kazi yanaenda kuimarika  na hivyo huduma ya maji inaendelea kuimarika katika wilaya ya Pangani na Korogwe katika vyombo vya Maji"

Kufwatia agizo la mkuu wa mkoa wa Tanga juu ya kuwasimamia Wananchi walioko katika  jumuia za watumia Maji  ngazi ya jamii 'CBWSO' Mhandishi Lugongo amesema "Suala la upandaji wa miti kwa ngazi za watumia maji  na CBWSO zote kuwa na vitalu vya upandaji miti sisi kama watumishi tumelipokea na tunaenda kulisimamia  kwa kushirikiana na viongozi wote  na itakapofika wakati wa kupanda basi tuweze kigawa miche kwa wananchi na mazingira yetu yaendelew kuwa salama lakini kikubwa zaidi tunakwenda kuhifadhibvyanzo vya maji" 

Katibu wa jumuia za watumia Maji Wilaya ya Korogwe  Mhandisi Kapota Abdi Kapota alisema kuwa suala la utunzaji wa vyanzo vya Maji ni la kila mwananchi ili kuendelea kukabiliana uharibifu wa vyanzo vya Maji ambao unaweza kupelekea changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.

"Pamoja na majukumu ya kusimamia jumuia za watumia Maji lakini tuna kazi ya kuhakikisha tunatunza vyanzo vya Maji na hii tunakwenda kutekeleza agizo la kuhakikisha kila CBWSO zilizoko mkoa wa Tanga zinaanzisha vitalu vya miti kwa kuwashitikisha Wananchi katika utunzaji wa mazingira" alisema Mhandisi Kapota.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »