Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndg. Mary Pius Chatanda(MCC) amewataka wanawake wafanyabiashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuachana na *mikopo ya kausha damu, ujinga na mwendokasi* inayowanyanyasa na kuwadhalikisha wanawake kutokana na muda wa marejesho na kiwango cha riba kuwa kikubwa na hivyo badala ya kujikwamua kiuchumi inaongeza umasikini zaidi.
Akizungumza katika Uzinduzi wa Umoja wa wanawake wafanyabishara masoko yote katika Jiji la Dodoma (UWAWAMA), uliofanyika katika ukumbi wa Roma Complex , tarehe 01 Novemba, 2024 amewataka wanawake wafanyabiashara kuachana na mikopo ya kausha damu na kujiunga na vikundi ili kupata Mikopo ambayo inatolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
*”Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan imerejesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa utaratibu ulioboreshwa zaidi ikiwemo kutumia benki kwa Halmashauri 10 za majaribio ikiwemo za Dodoma”* alisema Chatanda.
Kuhusu mikopo ya kausha damu, aliwataka wafanyabiashara kuachana nayo kwasababu inarudisha uchumi wa nchi nyuma na mwanamke anashindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na masharti magumu ya riba na muda uliwekwa katika mikopo hiyo.
*”Sasa nawahimiza kuchangamkia fursa ya mkopo usio na riba tuliyopewa na serikali na kuondokana na mikopo ya kaushadamu, ujinga na mwendokasi inayowanyanyasa na kuwadhalilidha wanawake kutokana na utaratibi wa mikopo hiyo ikiwemo muda wa marejesho na kiwango kikubwa cha riba kuwa kikubwa hivyo badala ya kujikwamua kiuchumi inaongeza umaskini zaidi” alisisitiza Chatanda.*
Katika kuhamasisha wanawake walengwa wa mikopo, Chatanda alitoa rai kwa viongozi wanawake kuhamasisha wachangamkie fursa ya mikopo inayotolewa na serikali. *”Natoa wito kwa viobgozi wanawake kuhamasisha walengwa wa mikopo hii wachangamkie fursa ya mikopo inayotolewa na serikali yao”.*
Aidha, amewashukuru wanawake wa nchi nzima kwa kuitikia wito wa kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
*”Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TAMISEMI inaonesha wanawake walioandikishwa ni alilimia 51.29 na asilimia 48.71 ni wanaume.Asanteni sana wanawake kwa kuiheshimisha serikali, kiongozi qetu mkuu wa Nchi, pamoja na mimi mwenyekiti wenu, ambaye wakati wa ziara zangu zote nimekuwa nikiwasihi wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha”* alieleza Chatanda.
Uzinduzi wa umoja wa wanawake wafanyabiashara masoko yote katika jiji la Dodoma ulihudhuriwa na wanawake wa masoko mbalimbali kama soko la Ndugai, Sabasaba, Mahengo, Machinga na Bonanza. Pia na vikundi mbalimbali kama Wanawake na Samia, wanawake na Nyerere, (Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Dodoma Jiji (JUWAKIDO).
Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndg. Mary Pius Chatanda akizindua Umoja wa wanawake wafanyabishara masoko yote katika Jiji la Dodoma (UWAWAMA), uliofanyika katika ukumbi wa Roma Complex , tarehe 01 Novemba, 2024.
Sehemu ya wafanyabiashara hao.
Baadhi ya viongozi wakishiriki uzinduzi huo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (wa pili kulia)na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (kulia).
EmoticonEmoticon