MILANGO YA RAIS SAMIA IKO WAZI, ANAWAKARIBISHA VIONGOZI WA DINI: DKT. BITEKO

October 27, 2024

 *Dkt. Biteko Amwakilisha Rais Samia Jubilei ya Miaka 50 ya AICT Magomeni, Achangia Milioni 100 Ujenzi wa Kanisa


*Atoa Wito kwa Viongozi wa Dini Kutimiza Kusudi la Mungu

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko tayari kuendelea kushirikiana na viongozi wa dini kwa ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu maendeleo na ustawi wa nchi.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba 27, 2024 Jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada maalum ya shukrani ya kuadhimisha miaka 50 ya Pastoreti ya AICT Magomeni.

“ Mhe. Rais anakumbuka namna mnavyomshirikisha katika masuala mbalimbali yanayohusu kanisa na kwa kweli milango yake iko wazi anawakaribisha wakati wowote ili muweze kutoa maoni yenu ya namna ya tunavyoweza kuiongoza nchi yetu,” amesema Dkt. Biteko.

Vilevile, Dkt. Biteko amesema maadhimisho ya jubilee ni kukumbuka wakati uliopita na kuangalia eneo gani lilifanyiwa kazi vizuri na lipi linahitaji kuboreshwa.

Amewahimiza waumini wa Kanisa hilo kujitoa kwa hali na mali katika kulijenga Kanisa bila kusubiri kesho “ Wito wangu kwetu tusiangalie leo tuangalie miaka 200 kanisa hili litakuwa wapi, tusisubiri kesho kwa kuwa hatuijui kesho itakuwaje. Fanya chochote unachoweza kufanya leo na kazi ya leo kisiwe kikwazo cha kazi ya kesho.” amesema Dkt. Biteko

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Kanisa hilo kuendeleza umoja miongoni mwa waumini wake na Watanzania na kusema kuwa wafuate misingi ya uanzilishwaji wake ambayo ni kujitawala, kujiendesha na kujieneza.

“ Hubirini upendo na msiruhusu mtu kutugawa wala kutubagua, Mungu ametupa nchi nzuri yenye rasilimali za kutosha, niwaombe Maaskofu na wachungaji wa Kanisa hili msivunjike moyo kusudi mliloitiwa na Mungu lisimamieni na waumini wa Kanisa hili tuwe sauti nzuri tuwasaidie viongozi wetu na tuwatie moyo,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, amelipongeza Kanisa la AICT kwa kuendelea kutoa hamasa kwa jamii na kuwakumbusha Watanzania kushiriki uchaguzi huo na kuchagua viongozi wenye sifa.

Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Mkuu wa AICT, Musa Magwesela amesema kuwa ibada hiyo ni muhimu kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa Magomeni mwaka 1974 limekuwa na mchango muhimu katika kutangaza injili.

“Kuna sababu 14 za kuhubiri utukufu na maajabu ya bwana, Kanisa hili la Magomeni kwa mujibu wa Zaburi ya 96 tumetumia njia 12 kuhubiri jina la bwana, ikiwemo kutumia nyimbo,” amesema Askofu Magwesela

Askofu Magwesela ameongeza kuwa wakristo wamehimizwa kutenda matendo mema, kutumia vipaji na kutumia karama zao.

Aidha, amesema Kanisa linatambua michango ya watu mbalimbali waliyotoa wakati wakifanya kazi katika Kanisa hilo la Magomeni huku akitaja majina ya baadhi ya wachungaji waliohudumia kanisa hilo“ Wito wangu tuenzi michango ya waliohubiri utukufu na maajabu ya bwana,” amebainisha Askofu Magwesela.

Vilevile katika kuunga mkono jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia, Askofu Magwesela amesema kuwa Oktoba 26, 2024 Kanisa hilo limegawa mitungi 20 ya nishati safi ya kupikia kwa jamii inayozunguka Kanisa.

Sambamba na ibada hiyo, Kanisa hilo limeendesha harambee kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kanisa, ofisi na madarasa ya watoto, ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha shilingi milioni 100.
 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko akizungumza katika sherehe za Kuadhimisha miaka 50 ya Kanisa la African Inland Charch Magomeni Jijini Dar Salaam.
 

 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko akipokea zawadi ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Askofu Musa Magwesela ya kutambua machango wake katika  katika sherehe za Kuadhimisha miaka 50 ya Kanisa la African Inland Charch (AICT) Magomeni Jijini Dar Salaam.

 


 

 Matukio mbalimbali katika picha ya sherehe za kuadhimisha miaka ya 50 ya Kanisa AICT Magomeni jijini Dar es Salaam.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »