Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Kilimo Husein Bashe (mb) atua kibabe Kisesa na kukutana na Mbunge wa jimbo hilo Luhaga Mpina ana kwa ana.
Amtaka mbunge huyo kuacha siasa katika zao la Pamba Kwani Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inahitaji kuona fedha zinazotengwa zinanufaisha wakulima.
Awaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa serikali inarejesha kitalu cha mbegu kuwapatia ruzuku ya dawa za wadudu katika zao la mahindi na pembejeo na mbegu katika zao la Pamba.
Wazee wa kimila wamsimika kuwa Mtemi (Chief) wa jimbo hilo.
Kihongosi aunguruma asema hataki siasa chafu mkoani humo kwani ametumwa kazi ya maendeleo na Rais Samia hivyo hayupo tayari kuona siasa katika kilimo.
Mpina asema yuko tayari kuweka tofauti zake na Bashe pembeni na kuungana katika masuala ya maendeleo na shughuli za serikali.
Bashe ametua jimboni humo katika mkutano na wananchi wa jimbo hilo wakati wa kufunga mashindano ya michezo mbalimbali ya Mwandoya na kupokelewa na mamia ya wananchi.
Ametumia fursa hiyo kukutana na Mbunge Mpina ambapo amemtaka kuacha siasa katika zao la Pamba kwa maslahi ya wananchi.
“Rais Samia amefanya kazi kubwa katika kilimo Mpina amesema hapa na mimi nataka nisisitize tuweke mambo mengine pembeni aache siasa na sitaki siasa katika zao la Pamba, nafahamu zipo changamoto lakini tulipotoka sio tulipo sitakubali mtu arudishe nyuma jitihada hizi wanaoteseka wananchi,”alisema.
Aidha amekabidhi trekta 40 kwa jimbo hilo na kuwataka maafisa kilimo na ugani kuacha kukaa mjini na kuishi vijijini ili waweze kuwasaidia wakulima utaalamu na kufikia malengo ya serikali ya kilimo chenye tija.
Amewashukuru wazee wa kimila kwa kumsimika kuwa mtemi wa jimbo hilo.
“Nami leo nimesimikwa kuwa mtemi wa Kisesa hivyo Mpina akinitambia pale bungeni kwa kuingia na fimbo ya uchifu nami nitaingia na yangu,”amesema.
Naye Mkuu wa mkoa huo Kennan Kihongosi amemuhakikishia Waziri Bashe kuwa yeye ndio mwenye dhamana na mkoa huo, hivyo hawezi vumilia watu wanaotafuta umaarufu katika siasa kuingiza masuala ya maendeleo.
“Nimetumwa kazi na Rais Dk. Samia, Simiyu ni ya kwanza ama ya pili katika kuzalisha pamba hivyo kwa wananchi ni zao la kiuchumi sitaki wanasiasa watumie zao hilo kutafuta umaarufu shida zinazosemwa katika zao hilo si za kweli wananchi wa Kisesa msikubali kutumika,”amesema
Naye Mbunge Mpina ametumia fursa hiyo kumkaribisha Bashe Kisesa na kueleza kuwa wanazo tofauti zao hali iliyowafikisha hadi Mahakamani lakini yupo tayari kushirikiana naye katika masuala ya utendaji wa serikali.
EmoticonEmoticon