DKT. JINGU ATAKA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUWAFIKIA WANANCHI

January 03, 2026


 ðŸ“Œ AKABIDHI PIKIPIKI  KWA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII SINGIDA.


Na Abdala Sifi WMJJWM- Singida 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanawafikia wananchi kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali na kuharakisha maendeleo ya wananchi. 


Dkt Jingu amesema hayo tarehe 2 Januari 2026 Mkoani Singida wakati akikabidhi pikipiki nane (8) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii ambazo zinalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. 


“Maafisa Maendeleo ya Jamii ni viungo muhimu sana kati ya Serikali na wananchi, hivyo niwaombe mkazitumie hizi pikipiki kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, kuwapa elimu ya fursa mbalimbali na kutatua changamoto zinazowakabili, kwa njia hiyo mtakuwa mmewasaidia kuongeza tija katika shughuli zao kwa maendeleo ya jamii”amesema Dkt Jingu. 


Aidha Dkt. Jingu amesema Serikali  inayooongozwa na Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  inatambua umuhimu wa Maafisa Maendeleo ya Jamii, hivyo itaendelea kuhakikisha inawapatia vitendea kazi ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo. 

Dkt.Jingu amewasihi Maafisa hao kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, kuhakikisha kila mwanachi anazitambua fursa hizo na kumwezesha kuziendea kwa ajili ya maendeleo yao. 

Amezitaja baadhi ya fursa hizo ni pamoja na mikopo kwa wafanyabiashara ndogondogo, uwezeshaji wanawake kiuchumi pamoja na fursa nyingine zinazotolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo. 

Kwa upande wake Afisa Maendeleo wa Mkoa wa Singida Patrick Kisango ameishurkuru Serikali kwa kuwapatia Maafisa Maendeleo ya Jamii pikipiki hizo na kwamba zitarahisisha utendaji wa kazi na kuharakisha maendeleo kwa wananchi. 

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2024/25, imetoa pikipiki (208) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mikoa mbalimbali.  




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »