WAZIRI GWAJIMA ATOA ONYO KUWATUMIA WATOTO KUCHEZA NYIMBO ZISIZO NA MAADILI KWENYE KUMBI ZA STAREHE

September 13, 2023


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuunda Kamati mtambuka na kuipa jukumu la kuja na mpango wa haraka na wa muda mfupi wa kudhibiti uvunjifu wa sheria ya mtoto na sheria nyingine za nchi zinazohusika na kutunza maadili.

Ametoa maagizo hayo leo Septemba 12,2023 Jijini Dar es Salaam, wakati alipokutana na wadau mbalimbali kufuatia kwa kushamiri vitendo vya kusambaa kwa maudhui yanayohusisha watoto wakicheza muziki usio na maadili kwenye kumbi za starehe.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Gwajima amesema kuwa kupitia mpango huo, wadau mbalimbali wakiwemo BASATA, TCRA, Wizara ya Katiba na Sheria, Bodi ya Filamu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wadau wengine muhimu waweze kushiriki kikamilifu katika kutokomeza yanayochochea mmomonyoko wa maadili kwa watoto wetu.

"Natoa siku 21 nipokee yatokanayo na kazi ya kamati hii ili nitoe mrejesho kwa jamii na kuandaa mjadala wa wazi ili jamii nayo itoe maoni yajumuishwe kwenye kazi ya kamati kwa ajili ya umiliki wa pamoja kama jamii". Amesema Waziri Dkt.Gwajima

Aidha Waziri Gwajima amewataka Wamiliki wa kumbi za starehe na Washereheshaji(MC) nchini, kuzingatia Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 ili kuwaepusha watoto na wimbi la mmomonyoko wa maadili.

Amesema kuwa washehereshaji na wamiliki wa kumbi za starehe, wapiga muziki (DJs) na Wazazi wana nafasi kubwa katika kumlinda mtoto ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili dhidi va watoto kupitia Sheria ya mtoto, Sura ya 13 kifungu cha 158 cha Katazo la Jumla.

"Pamoja na juhudi zinazofanywa a Wizara kwa kushirikiana na Wadau, bado baadhi ya familia na jamii wakiwemo wazazi na walezi hawatimizi wajibu wao kwa ufanisi kwenye malezi na makuzi stahiki ya watoto". Ameeleza

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »