RAIS DK.MWINYI KUSHIRIKI MKUTANO WA G77+CHINA NCHINI CUBA

September 12, 2023

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameondoka Zanzibar kuelekea Havana, Cuba kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la 77 na China (G77+ China) utakaofanyika tarehe 15 hadi 16 Septemba 2023.


Mkutano huo unalenga kukutanisha Mataifa yanayoendelea (Developing Countries) ili kujadili changamoto zinazoikabili dunia hasa baada ya kuathirika na UVIKO-19 na migogoro inayoendelea duniani pamoja na vikwazo mbalimbali vya kiuchumi.  

Hivyo, mkutano huo utajikita zaidi katika kutafuta namna bora ya kujenga ustahimilivu kupitia maendeleo ya sayansi na teknolojia na ubunifu ili kundi la G77 na China liweze kufikia malengo yake kwa pamoja.

Mkutano huu utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Current Development Challenges: The Role of Science, Technology and Innovation”.

Rais Dk.Mwinyi anatarajiwa kuhutubia mkutano huo na kuelezea vipaumbele vya Tanzania, pamoja na hatua zilizochukuliwa kukuza tafiti na kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu (STI) katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »