Na Fauzia Mussa, Maelezo
Wadau wa Maziwa wametakiwa kuchukua tahadhari wakati wanapozalisha na kusambaza bidhaa hiyo ili kuimarisha na kulinda Afya ya Mtumiaji.
Akiwasilisha mada ya udhibiti wa Usalama wa Bidhaa za Maziwa wakati wa mafunzo ya usalama wa chakula kwa Wafugaji,Wauzaji na Wasarifu wa Maziwa Ofisa Kutoka ZFDA Thamra Khamis Talib amesema maziwa hupitia hatua nyingi kabla ya kufika kwa mtumiaji ikiwemo ukamuaji na utunzaji hivyo mashirikiano ya pamoja yanahitajika ili kuhakikisha yanamfikia mtumiaji katika hali ya usalama.
Alisema maziwa yanaweza kuchafuka wakati yanapoingizwa katika vyombo visivyosafishwa vizuri ikiwemo chupa za plastiki na Vidumu hivyo aliwataka wadau hao kuacha kutumia vifaa hivyo kwani vinakua na vimelea vingi ambavyo haviwezi kuondoka kwa kukoshwa kwa maji na sabuni.
Aliongeza kuwa vifaa hivyo sio salama kwa afya ya mtumiaji na kuwataka wadau hao kuhifadhi maziwa katika chupa za vigae au vyombo vinavyoweza kuingia mkono wakati wa kusafisha.
Alifahamisha kuwa baadhi ya wauzaji hupokea maziwa safi kutoka kwa Mfugaji na kukaguliwa na ZFDA lakini mara baada ya ukaguzi huchafua maziwa hayo kwa maslahi binafsi na kuhatarisha afya za jamii.
“Ukaguzi wa ZFDA unafanyika wakiondoka tu wauzaji wanafanya ghushi watajaza maji waweke na samli ili yaonekane maziwa safi yenye mafuta kwa lengo la kupata faida zaidi kwa hali hii tutafika”alihoji Mwasilishaji
Alisema kuwa kuna baadhi ya Wauzaji huingiza vitu visivyohitajika katika maziwa kama samli , au siagi hali inayopelekea kuchafuka kwa bidhaa hiyo, hivyo aliwataka watumiaji kuacha kununua maziwa kama hayo kwani uchafuzi mwengine ni wawazi wala hauhitaji utaalamu na vipimo vya maabara.
“utayakuta maziwa juu yana rangi ya njano kabisa ya siagi unamimina chini kuna unga unga bado unaendelea tu kutumia maziwa hayo,tunavyoendelea kununua bidhaa hii kwa wauzaji kama hawa ndio tunawapa nguvu ya kuendelea kuharibu afya zetu”alisistiza Mwasilishaji huyo
Akifungua mafunzo ya kuwajengea uelewa Wadau hao juu ya usalama wa Chakula Mratibu wa mradi wa kudhibiti Sumu kuvu ZFDA Aisha Sleiman amesema wadau wengi wa maziwa hawana elimu hiyo, hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kujua njia sahihi ya kuhifadhi maziwa na kuhakikisha hayachafuki na kubaki salama hadi kufika kwa mtumiaji.
Alisema Serikali imeimarisha Idara ya udhibiti na maabara ya Dawa na Chakula Zanzibar kwa lengo la kumlinda mtumiaji , hivyo ZFDA itaendelea kukagua vyakula vyote ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha usama wa chakula kabla ya kuuzwa kwenye masoko ya ndani na nje ya Nchi.
Hata hivyo aliitaka jamii kushirikiana kwa pamoja kuweza kulinda na kuimarisha Afya ya mtumiaji kwa kutoa taarifa za uwepo wa chakula kisicho salama katika jamii
Washiriki wa mafunzo hayo Asia Mwinyi Bai, Suleiman Bakar simba na Salum Rehani Wameiomba Serikali kuwawakea viwanda vyenye mitambo ya kuchakatia maziwa na vifungashio vyenye ubora ili kuweza kuingiza bihaa zao katika hoteli za kitalii, nakuuzika nje ya Nchi.
Hata hivyo Washiriki hao wameiomba ZFDA kuandaa mafunzo kama hayo kwa mtumiaji ili kuongeza nguvu ya ulinzi wa afya za Jamii.
Awali walishukuru kwa kuwapatiwa mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliwashirikisha wadau wa maziwa kutoka Vikundi mbalimbali vya Wajasiriamali Mjini na Vijijini.
Wadau wa Maziwa wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya udhibiti wa bidhaa za chakula na mifugo huko Ofisi za Wakala wa dawa na chakula Mombasa Zanzibar .Mkaguzi wa chakula ZFDA Mwajuma Ali akiwasilisha mada ya usalama wa chakula wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa Wadau wa Maziwa juu ya udhibiti wa bidhaa za chakula na mifugo huko Ofisi za Wakala wa dawa na chakula Mombasa Zanzibar
Mratibu wa mradi wa kudhibiti Sumu kuvu ZFDA Aisha Sleiman akiwasilisha mada ya udhibiti wa sumu kuvu katika bidhaa za mifugo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wadau wa Maziwa juu ya udhibiti wa bidhaa za chakula na mifugo huko Ofisi za Wakala wa dawa na chakula Mombasa Zanzibar
PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR
EmoticonEmoticon