RAIS DKT SAMIA APONGEZWA KWA JUHUDI ZA KUENDELEZA MICHEZO, WAIPA TANO TAIFA STARS

September 11, 2023

 Na Mwandishi Wetu, Tanga


WABUNGE wa Kamati ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo, wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendeleza michezo nchini, kulikosabisha Taifa Stars kufudhu mashindano ya Afrika Mwakani (AFCON) nchini Ivory Coast.

Akizungumza katika majumuisho ya jumla baada ya Kamati hiyo kutembelea Kituo cha mafunzo cha TFF Mnyanjani, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko matokeo hayo ya kufudhu yamechagizwa na jitihada anazofanya Rais kwa shirikisho hilo pamoja na vilabu.

Amesema Kamati hiyo itaendelea kumuunga mkono na kumsaidia katika sekta hiyo ili iweze kuleta matokeo chanya ambayo yataifanya timu ya Taifa 'Taifa Stars' ione kawaida kufudhu fainali hizo.

"Tunampongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuchagiza katika michezo, matokeo haya ya kufudhu kwenda Ivory Coast Mwakani hayakuja hivi hivi ni ushirikiano wa Rais na wadau wengine wa michezo nchini, sisi Kamati yetu tutaendelea kumuunga mkono," amesema Husna.

Pia kamati hiyo imelipongeza Shirikisho hilo la michezo nchini kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miradi ya vituo hivyo vilivyojengwa Tanga na Dar es Salaam ikiwemo kuwa na Ligi bora yenye ushindani katika bara la Africa.

"TFF mmefanya vizuri katika miradi ya vituo hivi, lakini pia katika michezo mna Ligi bora ambayo sasa mnakwenda kumaliza lile la Tanzania kuitwa 'Kichwa Cha Mwendawazimu.

" Kamati hiii itaendelea kushirikiana na TFF katika suala la viwanja katika kila wilaya ili maeneo yatakayotengwa yatumike kwa ajili ya michezo na si vinginevyo."

Awali Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho hilo, Oscar Mirambo amesema taarifa ya mkakati wa muda mrefu wa Tanzania ni kupata vijana wenye vipaji ambao watapata mafunzo katika vituo hivyo ambako kwa Dar es Salaam pale Kigamboni watawekwa wachezaji wa rika tofauti kwa Wanawake na Tanga Mnyanjani watakaa wavulana wa umri tofauti.

Wakichangia baada ya wasilisho hilo baadhi ya wabunge wa Kamati hiyo waliipongeza TFF kwa malengo hayo lakini wakawataka wahakikishe wanalinda maadili ya vijana watakaokuwa katika vituo hivyo ili wasijiingize katika vitendo viovu ikiwa ni pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya na ndoa za jinsia moja.

Mbunge wa Magomeni Visiwani Zanzibar, Mwanahamisi Ali Kassim, licha ya kumpongeza Rais kwa kutoa fedha kuzisaidia timu za Simba na Yanga kununua magoli waliyofunga katika mashindano ya vilabu msimu uliopita halikuwa jambo dogo.

"Tumpongeze Rais kile kidogo alichotoa kwa timu zetu tumuungeni mkono na zile fedha zitumike vizuri tusimuangushe," alisema mbunge huyo na kulitaka shirikisho lihakikishe linalinda nidhamu kwa vijana.

Yanga iliyofunga magoli 15 ilipokea kiasi cha shilingi milioni 115 huku Simba iliyofika robo fainali ya Ligi ya Mabigwa Afrika ilifunga magoli 11 na kupata fedha za Rais kiasi cha shilingi milioni 55 na kufanya jumla ya fedha zote za Rais kuwa shilingi milioni 190 kwa magoli 26 yaliyofungwa na timu hizo.

Kamati hiyo ilionesha wasiwasi wa fedha kiasi Cha shilingi bilioni 4.513 zilizotumika kujenga viwanja viwili vya mpira pamoja na jengo la hostel la orofa mbili, jengo la utawala na jengo la mafunzo.

Makamo wa Rais wa Shirikisho hilo, Athumani Nyamlani aliwatoa wasiwasi wajumbe wa Kamati hiyo kwa kuwaeleza kwamba fedha hizo zimetumika kwa viwango vya Kimataifa vilivyowekwa na FIFA ikiwa ni pamoja na kutafuta wakandarasi waliojenga.

Nyamlani alisema uwepo wa vituo hivyo, utaleta tofauti mkubwa katika soka la Tanzania na kwamba uwepo wake vituo hivyo pia vitatumika kufunza waamuzi, wachezaji na viongozi wa mpira katika bara la Afrika.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA, ameiongeza Kamati hiyo na kueleza maagizo waliyotoa watayafanyia kazi ikiwemo Kituo Cha michezo cha Malya kilichopo jijini Mwanza kinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali.








Share this

Related Posts

Previous
Next Post »