KAMISHNA LUOGA ASISITIZA MAADILI NA UWAJIBIKAJI SEKTA YA NISHATI

February 03, 2026


Na Mwandishi Wetu


Mwenyekiti wa Kamati za Maadili za Wizara ya Nishati na taasisi zake, ambaye pia ni Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amewataka wajumbe wa kamati hizo kuzingatia uwajibikaji, maadili, uwazi na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi mahali pa kazi.


Mhandisi Luoga ameyasema hayo Februari 3, 2026 mkoani Morogoro  akifungua kikao kazi cha wajumbe wa Kamati za Uadilifu kutoka Wizara ya Nishati, taasisi zilizo chini ya wizara hiyo pamoja na kampuni zake tanzu.

Amesema kikao hicho kinalenga kuimarisha uwajibikaji na maadili kazini, kuongeza uelewa wa masuala ya kiutumishi pamoja na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwa wajumbe.


Kwa mujibu wa Kamishna Luoga, mafanikio ya sekta ya nishati yanategemea kwa kiasi kikubwa nidhamu kazini, matumizi sahihi ya rasilimali na uwajibikaji wa kila mtumishi wa umma, hivyo kamati za uadilifu zina wajibu mkubwa wa kusimamia misingi hiyo muhimu.

Ameongeza kuwa kuimarisha huduma kwa wateja katika Wizara ya Nishati na taasisi zake ni jambo la msingi huku akisisitiza kuwa watumishi wanapowahudumia wananchi kwa weledi, imani ya umma kwa Serikali huendelea kuimarika.


Katika hatua nyingine, Kamishna Luoga ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa kuendelea kufanya kazi kwa uwazi, hususan kupitia utaratibu wa kutangaza bei za mafuta kila mwezi, hatua inayosaidia wananchi kupata taarifa sahihi na kuimarisha uaminifu kwa taasisi za umma.

Vilevile, amepongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zake za kuboresha huduma kwa wateja, akieleza kuwa maboresho hayo yameongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kurahisisha mawasiliano kati ya shirika na wananchi, hali iliyochangia kupungua kwa malalamiko.


Katika kikao hicho, wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais,  Ikulu, Ofisi ya Rais,  Utumishi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na TAKUKURU waliwasilisha mada mbalimbali kuhusu rushwa mahali pa kazi na sheria za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma.


Mada hizo zililenga kuwajengea wajumbe uelewa mpana kuhusu changamoto za uadilifu na mbinu bora za kukabiliana nazo kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Taasisi zilizoshiriki kikao kazi hicho ni pamoja na TANESCO, TPDC, EWURA, PURA, PBPA, REA, pamoja na kampuni tanzu za GASCO, TANOIL, TGDC, TCPM na ETDICO, sambamba na watumishi kutoka Wizara ya Nishati.


&&&&

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »