WADAIWA SUGU WA MADENI YA “COMMODITY ORT SUPPORT (CIS) WATAKIWA KULIPA MADENI YAO NDANI YA SIKU 30

April 05, 2018





TANGAZO KWA WADAIWA SUGU WA MADENI YA “COMMODITY IMPORT SUPPORT (CIS)

Katika miaka ya 1980 hadi 2000 Wahisani walitoa fedha za kigeni kwa Serikali ya Tanzania kwa mpango maalum uliofahamika kama “Commodity Import Support (CIS)” kwa lengo la kuipa Serikali uwezo wa kuimarisha uchumi kwa kuzipatia Taasisi, Makampuni, Viwanda na wafanyabiashara uwezo wa kuagiza bidhaa na malighafi kutoka nje ya nchi, kwa kuwa wakati ule nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni.

Fedha za msaada za CIS zilitolewa kama mkopo wenye masharti nafuu kwa wanufaika, ambapo wakopaji walitakiwa kulipa deni bila kutozwa riba katika kipindi cha miezi 18. Kwa mujibu wa sheria ya CIS {The Commodity Import Support Regulation Act, CAP 261 R.E. 2002 (S. 8 (1) (b)}, mkopaji akichelewa kulipa katika kipindi cha miezi 18 tangu kupatiwa mkopo, atapaswa kulipa riba ya asilimia sawa na kiwango kinachotozwa na Benki Kuu ya Tanzania inapoikopesha Serikali (discount rate) katika kipindi husika. Zaidi ya makampuni 980 yalikopeshwa chini ya utaratibu huu. Pamoja na juhudi kubwa iliyofanywa na Serikali ya kuwataka wakopaji wote kurejesha mkopo huo, ikiwa ni pamoja na tangazo la tarehe 30 Desemba, 2015, bado urejeshaji wa mikopo hiyo umekuwa sio wa kuridhisha.

Ili kuhakikisha wadaiwa wote wanalipa mikopo yao, Serikali imeunda Kikosi Kazi ambacho kinajukumu la kufuatilia na kukusanya madeni toka kwa wadaiwa wote ili fedha hizo ziweze kutumika kwa miradi ya maendeleo. Serikali inawataka wadaiwa wote kulipa madeni hayo ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya kutolewa kwa tangazo hili. Kwa wote ambao hawatarejesha mikopo hiyo katika kipindi cha siku 30, majina yao yatatangazwa katika vyombo vya habari na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa maelezo zaidi, wasiliana na Kikosi Kazi, Wizara ya Fedha na Mipango, Dar es Salaam, chumba Na. 352, Simu Na. +255 739 40 30 25.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »