INUKA KUTUMIA MILIONI 40 KUTOA ELIMU YA MAGONJWA YA KIFUA KIKUU KWENYE MIKOA YA KILIMANJARO NA TANGA

April 06, 2018
MTANDAO wa Maendeleo ya Wanawake,Watoto na Elimu nchini (INUKA) umeanza kutoa elimu ya magonjwa ya kifua kikuu,saratani ya matiti na tezi dume kwa wakazi wa vijijini na shule kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.

Hayo yalisemwa na Mratibu wa Mtandao huo,David Msuya wakati akizungumza na Tanga Raha Blog ambapo alisema wametenga sh. milioni 40 kwa ajili ya kutoa elimu hiyo kwenye kuendesha mafunzo ya magonjwa hayo kwenye vijiji vilivyopo wilayani nane za mikoa hiyo miwili.

Msuya alisema kuwa lengo la kuendesha mafunzo hayo kwa wakazi wa vijijini ni kutokana na ukweli kwamba jamii inayoishi katika maeneohayo ni vigumu kufikiwa na mafunzo mbalimbali nahivyo kuwa na uhitaji mkubwa wa kupata elimu kama hizo.

Alisema kuwa jamii inayoishi vijijini itanufaika na elimu hiyo kwa kujengewa uwezo wa uelewa wa maambukizi ya magonjwa hayo na kuchukua tahadhali ya kujikinga nayo na hivyo kupunguza ongezeko la kifua kikuu,saratani ya matiti na tezi dume.

Mratibu huyo alisema kuwa lengo la kuendesha mafunzo hayo kwa jamii za vijijini na wanafunzi wa sekondari ni kuinusuru jamii hiyo ambayo ambayo imekuwa na
tatizo la elimu ya magonjwa hayo kutokana na kutofikiwa na wataalamu kwa urahisi na kwa wakati.

Hata hivyo alisema pamoja na serikali kujikita kwenye uhamasishaji wa masuala mbalimbali yanayohusu afya kupitia vyombo vya habari lakini jamii ya vijijini imekuwa vigumu kufikiwa kutokana na mazingira ya ufikaji wa taarifa hizo.

Msuya alizitaja Wilaya hizo ambazo zitanufaika na mafunzo hayo kuwa ni Handeni,Kilindi, Mkinga na Pangani kwa upande wa Mkoa wa Tanga naWilaya nyingine nne za Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande mwingine mratibu huyo alichukua nafasi hiyo kuwaomba wahisani kutoka mashirika na taasisi mbalimbali kusaidia gharama za utoaji wa elimu hiyo na kwamba kufanya hivyo licha ya kuisaidia serikali lakini pia watakuwa wameinusuru jamii na tatizo la kuathirika kwa magonjwahayo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »