Raisi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Ndugu Wallace
Karia amesema yeyote atakayebainika kufanya vitendo visivyo vya
kiungwana kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza inayoendelea TFF
haitasita kuwachukulia hatua.
Rais Karia alisema yapo malalamiko ambayo yanafanyiwa kazi
yanayohusu michezo iliyohusisha Dodoma Fc vs Alliance na Biashara Mara
vs Pamba ya Mwanza ambapo utaratibu utafuatwa na yeyote atakayebainika
hatua dhidi yake zitachukuliwa.
Ameongeza kuwa tayari amemuagiza Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Kidao
Wilfred kukutana na kamati ya Waamuzi ambao ndio wenye jukumu la masuala
yote yanayohusu waamuzi ili kuangalia kama Waamuzi wanaotumika wana
uwezo wa kuchezesha kwa kiasi gani.
Aidha Rais Karia amesema TFF inashirikiana na Taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) ili kudhibiti vitendo visivyo vya
kiungwana na Taasisi hiyo itapatiwa ratiba ya mechi zote ili iweze
kufuatilia kwa ukaribu.
Vilevile
amesema TFF na Bodi ya Ligi wanashirikiana kwa karibu kuhakikisha
anayeshinda ashinde kihalali kwa uwezo akitolea mfano namna mashindano
ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa namna yanavyochezeshwa kwa
haki na kuleta mvuto.
Amesema ni wakati wa kushirikiana kwa kila mmoja ili mpira uchezwe na kuondoa malalamiko ya kila wakati.