WAZIRI JAFO: Wakuu wa Wilaya Simamieni kazi zinazofanywa na TARURA

December 19, 2017
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Selemani Jafo amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote nchini kusimamia  kazi zinazofanywa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA)  ili kuleta matokeo tarajiwa  katika kukuza ustawi wa kiuchimi nchini.
Akifungua kikao cha Wakuu wa Wilaya nchini kote, Mhe. Jafo amewataka Wakuu wa Wilaya kwenda kusiamamia barabara hizo kwa ukaribu ili barabara zitakazo jengwa ziwe na ubora na zitakazo dumu kwa muda mrefu.
Mhe. Jafo amewaambia wakuu hao kuwa uanzishwaji wa Wakala utainua chachu ya uzalishaji wa mazao kutokana na usafiri wa uhakika, ambapo mkulima atakuwa na uhakika wakusafirisha mazao, lakini pia kupunguza gharama za usafiri lakini pia kuboresha hali za maisha za watanzania.
Amesema Serikali imekuwa na changamoto kubwa sana ambapo wakandarasi wanaopatiwa kazi za ujenzi wa barabara kutokuwa waaminifu na kujenga chini ya kiwango, rushwa , hivyo ni kazi ya Mkuu wa Wilaya kusimamia ili kubaini mapungufu hayo kwa haraka na kuokoa fedha za Serikali.
Amesema kuwa baada ya kuifahamu TARURA ni jukumu lao kuibua maovu kwa wafanyakazi wanaofanya maovu ili waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Amesema kuwa Wakuu wa Wilaya ni wawakilishi wa serikali katika maeneo yao, hivyo wanawajibu wa kusimamia kwa ukaribu zaidi katika usimamizi wa mradi ya Ujenzi wa Barabara nchini kwa kuzingatia kuwa asilimia 43 za barabara zinasimamiwa na TARURA zipo katika hali mbaya hivyo Mkuu wa Wilaya anajukumu la kusimamia kazi zinazotekelezwa kuanzia ngazi ya kata ili kuwa na kazi bora katika jamii. 
“Nimezunguka nchi hii karibu kila pembe ya nchi na kila nilipo Wakuu wangu wa Wilaya wamekuwa wakilia juu ya ubovu wa barabara, wengine kukiri kuumwa na migongo, alisema Jafo na kuongeza. “tunahitaji kuunganisha Vijiji, Wilaya na Mikoa kwa mtandao imara utakao wezesha vijiji vyote na maeneo yote ya vijijini na mijini vinafikika kwa wakati” Jafo.
Aidha  mbali  na kuhimiza kusimamia suala zima la barabara, Mhe.Jafo amerudia wito wa Waziri Mkuu wa kuwataka  waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na  Wakuu wa Wilaya kuzisiamamia Halmashauri ili ziweze kuchangia fedha kutoka katika mapato ya ndani.
Wakati huohuo Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara Vijijini na Mijini Bw. Victor Seif amesema imekabidhiwa mtandao wa barabara wenye jumla ya km 108,946.2 ambapo kati ya hizo km 52,946.2 zinatambulika kisheria na km 56,000 mchakato wa kuzihakiki ili zitambulike kisheria unaendelea.
Amesema hali ya mtandao wa barabara nchini hadi kufikia  Disemba, 2016 ilionyesha kuwa asilimia 22.6 ilikuwa na hali nzuri, asilimia 34.2 hali ya wastani na asilimia 43.2 hali mbaya.
Aidha vikao vya kujenga uelewa kuhusu majukumu ya TARURA nchini  vimeeshatolewa kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu  Tawala wa Mikoa,  Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waheshimiwa Madiwani, Kamati za kudumu za hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na  Kamati ya Serikali za Mitaa.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo katika kikao cha  Wakuu wa Wilaya kuhusiana na  kujenga uelewa wa majukumu ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA) katika ukumbi wa Hazina Dodoma, leo.
 Baadhi ya Wakuu wa Wilaya waliohudhuria katika kikao cha kujenga uelewa wa majukumu ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Dodoma, leo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »