Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. January Makamba akifungua kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa
Mazingira hii leo katika Ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma. Kikao hicho
kinajumuisha wakumbe kutoka sekta mbalimbali. Wengine katika picha ni Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Butamo Phillip na Katibu Mkuu Mhandisi
Joseph Malongo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. January Makamba akimkabidhi vitendea kazi mmoja ya wajumbe wa Kamati ya
Kitaifa ya Ushauri wa Mazingira hii leo katika Ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.
Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Butamo Phillip na Bw.
Richard Muyungi Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini - OMR
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. January Makamba akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya
Kitaifa ya Ushauri wa Mazingira mara baada ya ufunguzi uliofanyika katika
Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Ushauri wa Mazingira;
Mhe. Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira;
Naibu Katibu Mkuu,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira;
Ndugu wajumbe;
Wanahabari;
Mabibi na Mabwana.
Ndugu
wajumbe;
Kwanza kabisa,
napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupa afya
njema. Pia nawashukuru nyote kwa kukubali kuja kushiriki katika kikao hiki cha
uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Mazingira (The
National Environmental Advisory Committee), licha ya kwamba mnayo majukumu mengi maofisini kwenu. Tunatambua na
kuheshimu uwepo wenu hapa na ni ushahidi tosha kuwa sote tuko tayari kukaa
pamoja kujadili masuala yenye mustakabali wa Taifa letu. Nawashukuruni sana
wote.
Ndugu wajumbe;
Kama mnavyofahamu, nchi yetu inakabiliwa na changamoto
mbalimbali za uharibifu wa mazingira unaotishia juhudi za serikali na wadau
katika kufikia maendeleo endelevu. Baadhi ya changamoto hizi ni pamoja na: Uharibifu wa
mazingira utokanao na uvamizi wa wafugaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji;
Uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za kilimo kisichoendelevu kwenye
miteremko ya milima, mabonde na vyanzo vya maji; Uharibifu wa mazingira
utokanao na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa; upungufu wa maji ya
kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme; Uharibifu wa
mazingira ya vyanzo vya maji utokanao na moto; Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame katika maeneo mengi nchini; Uelewa
na ushiriki mdogo wa wananchi katika hifadhi ya mazingira; Migongano katika
matumizi ya ardhi baina ya wadau mbalimbali na uharibifu wa mazingira utokanao na shughuli za uchimbaji madini na uchafuzi wa mazingira utokanao na majitaka, taka ngumu na hatarishi
zitokanazo na sekta ya viwanda, kilimo na afya. Changamoto hizi za uharibifu wa
mazingira zimesababisha athari kadhaa kama vile mabadiliko ya tabianchi,
upotevu wa bioanuai za misitu na hivyo kuwepo kwa tishio la kutoweka kwa baadhi
ya jamii ya mimea miti na viumbe wengine.
Ndugu wajumbe;
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekua
ikibuni na kutekeleza hatua kadhaa zenye lengo la kukabiliana na changamoto
hizo za uharibifu wa mazingira nchini. Katika kipindi hiki kifupi cha Serikali
ya awamu ya tano, tumekabiliana na changamoto hizo na baadhi ya mafanikio
yamepatikana ambayo ni pamoja na: Kuanzishwa kwa Carbon Monitoring Centre – SUA; Jumla ya
vyeti zaidi ya mia nane (800) vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM)
vimeidhinishwa; Viwanda vimeweka mifumo ya kutibu Maji taka na kupunguza
uchafuzi wa Mazingira kama vile Viwanda vya Saruji vya Twiga na Lake Cements;
Makampuni binafsi mbalimbali yamekidhi matakwa ya hifadhi ya mazingira; Kamati
ya Kitaifa ya kusimamia matumizi ya Bioteknolojia ya kisasa imezinduliwa; Mfuko
wa mazingira umeanzishwa; Mchakato wa kufanya mapitio ya Sera mpya ya Mazingira
unaendelea; Siku ya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi imepitishwa
(Gazetted) na kuwa sheria; Miradi ya hifadhi ya Mazingira na Mabadiliko ya
Tabianchi (Climate Change) yenye thamani ya zaidi Dola milioni Mia moja
imeandaliwa na inatafutiwa fedha kwa ajili ya utekelezaji; Serikali kupitia Ofisi
Ya Makamu wa Rais imeandaa miradi minne (4) yenye jumla ya Dola za Marekani
milioni 28. Fedha za utekelezaji wa Mradi huu zinategemewa kutoka katika Mfuko
wa Dunia wa Mazingira (Global Environment Facility – GEF). Miradi hiyo ni
pamoja na:
(a) Mradi wa Kukabiliana na Kasi ya Uharibifu wa
Ardhi na Kuongeza Upatikanaji wa Chakula katika Maeneo Kame Nchini (Reversing
Land Degradation Trends and Increasing Food Security in Degraded Ecosystems of
Semi-arid areas of Tanzania. Mradi huu una thamani ya Dola za Marekani Milioni
7.1. Utekelezaji utafanyika kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa Maendeleo ya
Kilimo (International Fund for Agricultural Development – IFAD). Utekelezaji wa
Mradi huu unatarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa
mwaka 2017.
(b) Mradi
Kuhimili mabadiliko ya Tabianchi katika Mifumo-ikolojia ya maeneo ya Vijijini
(Ecosystem Based Adaptation for Rural
Resilleience). Thamani ya Mradi huu ni Dola za Marekani milioni 7.57.
Utekelezaji utafanyika kwa kushirikiana na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa
(United Nations Environment Programme - UNEP). Mradi huu uko katika hatua za
awali za utekelezaji.
(c) Mradi wa
Kusaidia Utekelezaji wa Usimamizi wa Urejeshwaji wa Maeneo ya Mifumo-ikolojia
yaliyoharibika na kuboresha uhifadhi wa bioanuai (Supporting the Implementation
of Integrated Ecosystem Management Approach for Landscape restoration and
Biodiversity Conservation in Tanzania). Thamani ya Mradi huu ni Dola za
Marekani milioni 12.14. Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (United
Nations Environment Programme - UNEP). Utekelezaji wa Mradi huu unatarajiwa
kuanza rasmi katika kipindi cha mwaka 2017/18.
(d) Mradi wa
Usimamizi Endelevu wa Bonde la Ziwa Nyasa (Sustainable Land Management of the
Lake Nyasa Catchment). Thamani ya Mradi huu ni Dola za Marekani milioni 1.3.
Utekelezaji utafanyika kwa kushirikiana na Programu ya Mazingira ya Umoja wa
Mataifa (United Nations Envionment Programme - UNEP). Mradi huu pia uko katika
hatua za awali za utekelezaji.
Ndugu wajumbe;
Uzinduzi wa Kamati hii ya Ushauri wa Mazingira
umekuja muda muafaka wakati ambapo serikali inaendelea kushughulikia changamoto za uharibifu wa mazingira nchini ambazo
zinakua kila kuchapo. Ujuzi,
utaalamu, weledi na uzoefu wenu katika nyanja mbalimbali unategemewa sana
katika kutoa ushauri muafaka katika kukabiliana na changamoto zinazotukabili.
Ni matumaini yangu kwamba tutashirikiana vyema katika kazi hii ili kutimiza
azma ya serikali ya kuwa na Tanzania ya viwanda bila kuathiri mazingira yetu na
hivyo kuchangia katika maendeleo endelevu kwa taifa zima. Sisi kama wajumbe wa
Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa mazingira tunategemewa kutoa ushauri ambao
utasaidia kujikwamua na changamoto za uharibifu wa mazingira nchini. Ni lazima sasa kama taifa tuchukue hatua zenye
mtizamo mpya katika kukabiliana na changamoto hizi ili kutimiza azma ya
matarajio ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda.
Ndugu wajumbe;
Uwepo wenu katika Kamati hii unatarajiwa kusaidia
sana katika kushauri mbinu na mitazamo mipya na bora zaidi ya jinsi ya
kukabiliana na kupunguza changamoto za uharibifu wa mazingira nchini. Hili sina
shaka nalo kwani nikiangalia mchanganyiko wa wajumbe wa Kamati hii pamoja na
uwakilishi mpana kutoka kwenye sekta mbalimbali, ujuzi, majukumu na uzoefu mlio
nao naamini kabisa Kamati hii itakua na mchango mkubwa katika kutekeleza
majukumu yake.
Ndugu wajumbe;
Jukumu lililo mbele yenu ni kushauri na kusaidia katika kutekeleza Sera,
Sheria, Mikakati na Mipango tuliyojiwekea. Ni matumaini yangu leo mtapata fursa
ya kupitishwa kwenye masuala mbalimbali ambayo ninyi kama Kamati ya Ushauri kwa
Waziri mwenye dhamana ya Mazingira ningependa kupata ushauri wenu wa kitaalamu
baada ya kuyajadili kwa pamoja. Mtakavyoendelea kufanya hivyo, Kamati hii
itakua na mchango mkubwa katika kushughulikia changamoto za mazingira bila
misigano. Napenda kusisitiza kwamba hifadhi ya mazingira na matumizi bora ya
rasilimali zake ndio msingi wa maendeleo endelevu, na ni wajibu wetu sote. Sote
tuchangie katika namna bora ya kukabiliana na changamoto za uharibifu wa
mazingira nchini kwa maendeleo endelevu bila kujali unatoka sekta gani kwani
ushauri wenu utatufanya tutoke pale tulipokwama.
Baada ya kusema hayo nawatakia heri katika kazi iliyo mbele yenu na ninayo
furaha kuizindua rasmi Kamati hii ya Ushauri wa Mazingira (National
Environmental Advisory Commitee – NEAC).
ASANTENI SANA