TABIA ZA KUEPUKA ILI UWE MWENYE AFYA BORA

December 19, 2017

Na Jumia Food Tanzania


Chakula huupatia mwili virutubisho ili uweze kufanya kazi kwa ufasaha. Chakula pia ni sehemu ya mila na utamaduni wa watu. Hii inamaanisha kwamba kwa baadhi ya watu chakula kina muunganiko mkubwa na hisia zao. Kwa watu wengi, kubadili tabia na mienendo ya kula vyakula vya aina fulani ni jambo gumu kutekelezeka.

Kuna uwezekano umekuwa na aina fulani ya tabia za vyakula unavyokula kwa muda mrefu ambazo haujagundua kama si nzuri kiafya. Au, tabia hizo zimekuwa ni sehemu ya maisha yako ya kila siku, kwa hiyo hauzifikirii sana.

Katika maisha ya sasa imekuwa ni changamoto sana kuthibiti aina ya vyakula tunavyokula ambavyo kwa mujibu wa wataalamu wa afya ni hatari. Jumia Food ingependa kukushauri juu ya hatua za kufuata ili kuachana na tabia au mienendo ya vyakula unavyokula na kukudhuru kiafya kwa namna moja ama nyingine.

Fuatilia mwenendo wa tabia zako. Ni jambo zuri kufuatilia tabia za vyakula unavyopendelea kula. Unaweza kufanya hivi kwa kurekodi kwenye kijitabu kidogo ndani ya kipindi cha muda fulani kama vile kwa wiki. Andika chakula unachokula, kwa kiwango gani, na ni muda gani huwa unakula. Pia weka maelezo kuwa ulikuwa kwenye mazingira na hali gani, kama vile njaa, msongo wa mawazo, uchovu, au kuboreka. Kwa mfano, inawezekana ulikuwa upo kazini umechoka na ukaamua kununua soda au chokoleti kujiburudisha. Mwisho wa wiki, pitia kijitabu chako ili kujua mwenendo wa tabia za ulaji wako. Amua ni tabia zipi ungependa kuzibadili.    

Tafakari. Baada ya kufuatilia na kujua mwenendo wa tabia zako, ni vema kutafakari juu ya mambo yanayokupelekea kuwa na tabia hizo. Je, kuna mazingira ambayo ukiwa karibu nayo yanakufanya ule au uchague aina fulani ya chakula huku ukiwa hauna njaa? Je, ni namna unavyojisikia ndiko hukufanya ule aina fulani ya chakula? Pitia kwa makini kumbukumbu zako na kujua ni mara ngapi tabia hizo huwa zinajirudia. Kwa mfano, kula pale unapokiona kile chakula unachokipenda unapopita dukani au kukiona kwenye tangazo luningani au kuboreka na mazingira fulani au kutokuwa na mpango wa kupika usiku. Anza kwa kujikita zaidi kwenye tabia ambazo hujirudia zaidi ndani ya wiki, kisha fikiria namna ya kuziepuka hizo tabia kama vile kutopita karibu na sehemu ambapo wanauza vyakula unavyovipenda au kuamua mapema mpango wa kula usiku.    

Badili tabia zako za zamani. Ukishatafakari mwenendo mbaya wa tabia za ulaji wako kinachofuatia ni kufanya mabadiliko. Kwa mfano, kama huwa unapendelea kunywa soda pale unapochoshwa na kazi badili na kunywa maji au hata badili shughuli unayoifanya ndani ya muda mfupi. Mbali na kubadili tabia, kama ni vigumu kubadili moja kwa moja, angalau punguza kiwango cha tabia hiyo. Kama ulikuwa unatumia chakula hiko kwa kiwango kikubwa, punguza kidogo.  

Zifanyie mazoezi tabia mpya. Inaweza kuchukua muda mrefu kubadili tabia za zamani, na zile za kiafya zaidi. Kumbuka, ilikuchukua muda mrefu kuwa na tabia ulizonazo. Hivyo hivyo, itakuchukua muda kuzibadili pia. KWA HIYO USIKATE TAMAA.

Kwa kumalizia, Jumia Food inakusisitiza kwamba endapo utajikuta unaanza kuzifikiria tabia za zamani, tafakari kwa makini ni kwanini unataka kuzirudia. Jaribu tena kuzibadili. Kuteleza kwenye kufanya jambo fulani hutokea, na hakumaanishi kwamba umeshindwa. Endelea kujaribu tena na tena! 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »