FCT YAPEWA MAELEKEZO MAPYA KUHUSU ULINZI WA WALAJI NA BIASHARA NDOGO

December 23, 2025

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi ,akizungumza wakati wa ziara yake katika Baraza la Ushindani (FCT) Jijini Dar es Salaam.

....

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi (Mb), ameliagiza Baraza la Ushindani (FCT) kuendelea kusimamia na kulinda ushindani wa haki ili kuondoa vitendo vya ukiritimba, hususan katika suala la kupandisha bei za bidhaa na huduma.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Baraza la Ushindani Desemba 22, 2025 Jijini Dar es Salaam akisisitiza kuwa ushindani wa haki ni msingi muhimu wa ukuaji wa biashara, kwani vitendo vya ukiritimba vimekuwa vikiathiri biashara nyingi na walaji.

Ameeleza kuwa biashara zinapaswa kufanyika kwa kuzingatia ulinzi wa walaji, ambapo bei za bidhaa na huduma ziwe za haki, bidhaa ziwe na ubora, na uchunguzi wowote ufanyike kwa haki na kwa kuzingatia misingi ya kisheria.

Mhe. Katambi amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa kuboresha sera rafiki, kufanya marekebisho ya sheria na kuendelea na maboresho ya mazingira ya biashara ili kuhakikisha Tanzania inakuwa mahali salama na rafiki kwa kufanya biashara bila kuweka vikwazo kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa haki katika utatuzi wa migogoro ni kipaumbele, kwa kulinda muda, heshima na maslahi ya wawekezaji na kusimamia sheria za ushindani, ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kumlinda mlaji ili awe mnufaika mkuu wa shughuli za kibiashara.

Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani Jaji Rose Ibrahim, Dkt. Onesmo Kyauke amesema Baraza la Ushindani lina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha malengo ya sera ya ushindani nchini yanatekelezwa kwa ufanisi, hususan kupitia usikilizaji wa rufaa na mashauri yanayotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani pamoja na mamlaka za udhibiti wa soko.

Amesema hatua hiyo inasaidia kujenga mazingira bora ya biashara, kuvutia uwekezaji na kulinda maslahi ya walaji na washiriki wote wa soko.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »