WIZARA TATU KUIMARISHA KILIMO MAGEREZA

February 03, 2026


Na Mwandishi Wetu,DODOMA

Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo na ufugaji katika Jeshi la Magereza ili kuliwezesha jeshi hilo kutumia maeneo inayomiliki kwa kilimo chenye tija huku ikiweka wazi kuyatafutia hati maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na Jeshi hilo, lengo ikiwa kukuza kipato kwenye kilimo ikiwemo kulisha wafungwa na kufanya biashara ya mazao hayo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi wakati wa Kikao cha kwanza na Uongozi wa Juu wa Jeshi la Magereza, Maafisa, askari na watumishi raia, kilichofanyika Makao Makuu ya jeshi hilo, Msalato jijini Dodoma ambapo aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Ayoub Mohamed Mahmoud.

“Ni jukumu letu sasa kuhakikisha maeneo yetu sasa tunayatambua mipaka yake, yale yasiyo na hati zijulikane ziko wapi na kama hazipo tutafute hati na yale yanayofaa kwa kilimo tuyainishe na tuyanakiri ili tujue tunaweza tunaweza kufanya nini.Wizara ya Mifugo na Uvuvi iko tayari kufanya kazi na sisi, Wizara ya Kilimo pia iko tayari kuhakikisha tunafanya kilimo kikubwa chenye tija na kitakachojibu haja na matamanio ya Jeshi la Magereza, lakini pia kupata kipato na kupunguza nakisi ya mahitaji, suala la upungufu wa wazabuni umelisema hapa CGP (Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza), hatuhitaji tena wazabuni kwasasa kama tutajipanga vizuri,tutawahitaji kwa hatua ya sasa lakini kwa baadae haitakuwepo kwasababu tuna magereza sehemu mbalimbali ambayo yanaweza kuzalisha mazao yanayokubali kuota sehemu husika.” Amesema Waziri Katambi

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema serikali itakazia zaidi masuala ya teknolojia katika viwanda, kilimo na mifugo ili kuweza kuleta ufanisi zaidi katika utendaji wa Jeshi la Magereza ambapo aligusia dhana hiyo kuwepo katika Dira ya 2050.

Nae Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu amesema Jeshi linatoa mafunzo ya ujasiriamali katika Gereza la Arusha ambapo jumla ya wafungwa 209 walihitimu mwaka jana(2025), Chuo cha Uhasibu Arusha ambapo pia ameweka wazi mahusiano ya Jeshi la Magereza na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) huku jumla ya wafungwa 201 walihitimu mafunzo na kupewa vyeti na mamlaka hiyo.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »