DKT .BATILDA BURIAN TANGA IPO TAYARI KUMPOKEA MWENGE WA UHURU 2026

June 16, 2026


Na Paskal Mbunga,TANGA

 Mwenge wa Uhuru 2026 unatarajiwa kuwasili mkoani Tanga  Juni 17 mwaka huu, ambapo utakimbizwa katika halmashauri zote 11 za mkoa huo na kukagua, kuzindua pamoja na kuweka mawe ya msingi katika miradi 73 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 27.7.

Akizungumza leo na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, alisema Mwenge wa Uhuru utapokelewa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mpya, Kijiji cha Mtoro, Kata ya Tunguli wilayani Kilindi ukitokea Mkoa wa Morogoro.

Alisema baada ya mapokezi hayo, Mwenge utakimbizwa kwa umbali wa kilometa 1,340 kupitia halmashauri zote za Mkoa wa Tanga kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Kilimanjaro Juni 28 mwaka huu katika Uwanja wa Shule ya Msingi Hedaru.

Dk. Burian alisema kati ya miradi 73 itakayofanyiwa kazi na Mwenge wa Uhuru, miradi 34 itawekewa mawe ya msingi, miradi 26 itafunguliwa na kuzinduliwa, miradi 11 ya vijana itakaguliwa pamoja na miradi miwili ya sekta ya maji.

Alifafanua kuwa miradi hiyo ina thamani ya Sh bilioni 27.76, ambapo Sh milioni 300.6 ni nguvu za wananchi, Sh bilioni 1.27 ni michango ya halmashauri, Sh bilioni 10.7 ni fedha za Serikali Kuu na Sh bilioni 15.47 ni mchango wa wahisani.

Akizungumzia kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu inayosema, “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo,” Dk. Burian alisema mkoa umejipanga kuhakikisha wananchi wa makundi mbalimbali wanashiriki kikamilifu katika shughuli zote za Mwenge.

Alisema viongozi wa serikali, watumishi wa umma, viongozi wa dini, wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu pamoja na makundi mengine wamehamasishwa kushiriki kikamilifu kuanzia mapokezi hadi makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru.

Aidha, wananchi watapata fursa ya kuushika na kuukimbiza Mwenge huo kama sehemu ya kuimarisha mshikamano, umoja wa kitaifa na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Mbali na kuhamasisha maendeleo, Mwenge wa Uhuru utaendelea kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, malaria, VVU/UKIMWI, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na umuhimu wa lishe bora kwa jamii.

Dk. Burian aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kwa wingi katika maeneo ya mapokezi, miradi na mikesha mbalimbali ili kushiriki shughuli za Mwenge wa Uhuru na kufaidika na ujumbe wake.

Alisema mkoa umejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanapata burudani na hamasa kupitia ushiriki wa wasanii na vikundi vya sanaa vitakavyoshiriki katika maeneo yote ambayo Mwenge wa Uhuru utakesha.

Kwa ujumla, alisema maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2026 yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha na Mkoa wa Tanga uko tayari kwa shughuli zote za mbio hizo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »