LINDI,MTWARA,KAGERA NA RUKWA KUPATA UMEME WA GRIDI NDANI YA MWAKA WA FEDHA 2026/2027

June 22, 2026




Serikali imesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 itatekeleza miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Kagera na Rukwa kwenye gridi ya taifa ya umeme ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hiyo nchini.


Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma  Juni 22, 2026, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema umeme si anasa tena bali ni hitaji la msingi kwa maisha ya wananchi jambo linaloiifanya Serikali kuendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta hiyo.



Amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini ili kuhakikisha nishati hiyo inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali.


Waziri  Ndejembi ameeleza kuwa umeme unaozalishwa katika Bwawa la Julius Nyerere unasafirishwa kupitia Chalinze kuelekea Morogoro na Dodoma, huku pia ukiunganishwa kwenye njia ya usafirishaji umeme ya Zuzu ili uweze kufika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Geita na Mwanza.


Ameongeza  kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali itahakikisha mkandarasi anayetekeleza mradi wa njia ya umeme ya Songea–Tunduru–Masasi–Mahumbika anatekeleza kazi kwa wakati huku Serikali ikiendelea kutoa malipo  yatakayomwezesha mkandarasi huyo kufanya kazi bila kukwama na hivyo kuwezesha mikoa ya Lindi na Mtwara kupata umeme kutoka gridi ya taifa.


Aidha, amesema Serikali inaendelea kukamilisha miradi ya njia za kusafirisha umeme kutoka Iringa kwenda Mbeya, Songwe na Rukwa pamoja na mradi wa Benako–Kyaka ambao unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo husika.


Kwa upande wa usambazaji wa umeme vijijini, Mhe.Ndejembi amesema Serikali imepanga kupeleka umeme katika vitongoji 9,009  huku idadi ya vitongoji vitakavyofikiwa na huduma hiyo ikiendelea kuongezeka katika miaka inayofuata.


Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.


“Ni kazi kubwa ambayo inakwenda kufanywa, lakini Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya umeme wa uhakika." Amesisitiza Waziri Ndejembi

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »