TATIZO LA UMEME MTWARA NA LINDI: MAFUNDI WA TANESCO WAFANIKIWA KUWASHA MASHINE MOJA

October 17, 2017
Mafundi wakiratibu zoezi la ukarabati wa mshine
NA K-VIS BLOG, MTWARA

SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco), limefanikiwa kukarabati mashine namba 6 iliyokuwa imeharibika na kuiwasha kwa ajili ya kutoa huduma ya umeme kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Hatua ya kuwashwa kwa mtambo huo ni juhudi za shirika hilo za kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwa wananchi kusini  huku ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Nishati,  Dk. Medard Kalemani alipotembelea Kituo cha kufua umeme kwa gesi .

Akizungumza leo mjini hapa, Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Mhandisi Dk. Tito Mwinuka ambaye amepiga kambi mkoani humo pamoja na watalaamu wengine, alisema kuwa mitambo iliyokuwa ikifanya kazi ilikuwa minne lakini baada ya juhudi kubwa za wataalamu wa Tanesco hadi kufikia jana jioni wamefanikiwa kuwasha mashine hizo zenye uwezo wa kuzalisha Megawati 16.

“Tanesco tumeshagiza vipuri vya aina mbalimbali ili kutengeneza mashine hizi na pia Shirika katika kuhakikisha kazi inakwenda kwa kasi zaidi itaongeza nguvu ya wataalamu kutoka vituo vingine vya TANESCO hapa nchini.

“Tunawaomba wateja wetu wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuendelea kuwa wavumilivu wakati uongozi wa Shirika, Kanda na Mkoa ukiendelea na juhudi za kumaliza kabisa upungufu wa umeme katika mikoa hii,” alisema Dk. Mwinuka.

Alisema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kwa mikoa hiyo, alisema Shirika limeshaanza taratibu za kupata Megawati nne za haraka kwa kuagiza mitambo mwili mipya.

“Tuna imani kubwa na wafanyakazi wa Kituo cha kufua umeme wa gesi cha Mtwara na wataweza kukarabati mitambo yote pindi vipuri vitakapowasili,” alisema

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo amewashukuru wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwa uvumilivu waliouonesha katika kipindi cha matengenezo ya mitambo hiyo

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Tito Mwinuka, (wakwanza kushoto), na viongozi wengine wa Shirika hilo, wakifuatilia maendeleo ya ukarabati wa mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara leo Oktoba 17, 2017.
Mafundi wa TANESCO wakiendelea na ukarabati wa mshine.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »