Precision Air yaongeza nguvu udhamini Rock City Marathon

October 17, 2017

Meneja Masoko na Mahusiano wa Shirikala la Ndege la Precision Air Bw Hillary Mremi (wa pilikushoto) akikabidhi mfano wa tiketi ya ndege kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio za Rock City Marathon, Bw Zenno Ngowi ( wa pili kulia) ikiwa ni ishara ya udhamini wenye thamani ya Sh 20 milioni kwa ajili ya mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Octoba 29 jijini Mwanza. Wengine ni pamoja na Mratibu wa mbio hizo kutoka Kampuni ya Capital Plus, Bw Bidan Lugoe (wa tatu kushoto) pamoja na maofisa wa makampuni hayo mawili.
Meneja Masoko na Mahusiano wa Shirikala la Ndege la Precision Air Bw Hillary Mremi akizungumza wakati wa makababidhiano hayo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Bw Zenno Ngowi pamoja  na Mratibu wa mbio hizo kutoka Kampuni ya Capital Plus, Bw Bidan Lugoe
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Bw Zenno Ngowi (katikati) akizungumzia udhamini huo. Kwa mujibu wa Ngowi udhamini huo unamaanisha kwamba uhusiano wa Precision Air na wateja wake hautaishia  ndani ya ndege bali utaendelea zaidi hadi kwenye mitaa, fukwe, viwanja vya michezo na sehemu zote za utalii katika jiji la Mwanza na Kanda ya Ziwa yote.
Mratibu wa mbio hizo kutoka Kampuni ya Capital Plus, Bw Bidan Lugoe (katikati) akizungumzia udhamini huo. Kwa mujibu Lugoe maandalizi yanaendelea vizuri na kwamba wamejipanga kupokea washiriki zaidi ya 4,000 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo viongozi na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.
 
 

SHIRIKA la ndege la Precision Air leo limetangaza udhamini wake wenye thamani ya Sh 20 milioni kwa ajili ya mbio za Rock City Marathon zinazotarajiwa kufanyika Octoba 29 jijini Mwanza.

Kwa udhamini huo, shirika hilo sasa linatambulika rasmi kama shirika maalumu la usafiri wa mbio hizo miongoni mwa wadhamini wengine zikiwemo kampuni za PUMA, Tiper, RedBull, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), New Mwanza Hotel, EF Out door, CF Hospital, KK Security, na kampuni ya uchapishaji ya SDS.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo ,Meneja Masoko na Mahusiano wa Precision Air Bw Hillary Mremi alisema udhamini huo kwa kiasi kikubwa umechagizwa na malengo ya mbio hizo yaliyojikita katika kutangaza utalii wa ndani kupitia mchezo wa riadha.

“Lakini pia kibiashara tunaona kwamba mara nyingi watu wanaopenda kushiriki riadha wamekuwa na ‘hobby’ pia kusafiri sehemu tofauti tofauti ndani na nje ya nchi hivyo ushiriki wetu kwenye mbio hizi utazidi kutukutanisha na kundi hili muhimu,’’ alibainisha.

Zaidi alionyesha imani kuwa mbio hizo zitakazofanyika jijini Mwanza zitakata kiu ya washiriki wake wakiwemo abiria wa shirika hilo kwa kuwa tofauti na mchezo huo, jiji hilo lina vivutio vingi vya kitalii ikiwemo fukwe za Ziwa Victoria, Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane na makumbusho ya kabila la wasukuma (Bujora)

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Bw Zenno Ngowi alisema kwao ni heshima kubwa kushirikiana na shirika hilo lenye heshima kubwa kwenye usafiri wa anga hapa nchini.

“Tunaamini kwamba ushirikiano huu na shirika hili linalotambulika kimataifa kwa ubora wa huduma zake za usafiri wa anga utaziweka na mbio hizi pia katika ngazi ya kimataifa.’’ alisema.

Aliongeza kuwa udhamini huo unamaanisha kwamba uhusiano wa shirika hilo na wateja wake hautaishia ndani ya ndege bali utaendelea zaidi hadi kwenye mitaa, fukwe, viwanja vya michezo na sehemu zote za utalii katika jiji la Mwanza na Kanda ya Ziwa yote.

Kwa upande wake Mratibu wa mbio hizo kutoka Kampuni ya Capital Plus, Bw Bidan Lugoe alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kwamba wamejipanga kupokea washiriki zaidi ya 4,000 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo viongozi na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.

“Kiukweli muitikio ni mkubwa sana kutoka ndani na nje ya nchi! Tofauti na washiriki wa kawaida kuna idadi kubwa ya viongozi wa serikali na kisiasa ambao tayari wamethibitisha ushiriki wao,’’ alisema Lugoe.

Aliwataja baadhi ya waliothibitisha ushiriki wao kuwa ni pamoja na baadhi ya wakuu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Makamanda wa Jeshi la Polisi pamoja na wale wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Akizungumzia usajili wa mbio hizo Bw. Bidan alisema kwa wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani wanaweza kujisajili kwa kuchukua fomu katika Ofisi za michezo wilaya zote za mkoa wa Mwanza, Ofisi za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga.

Sehemu nyingine ni pamoja na Uwanja wa Nyamagana, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Mwanza, Kituo cha michezo Malya, Shule ya Kimataifa ya Isamilo, New Mwanza Hotel na Ofisi za EF Out door zilizopo jingo la Rock City Mall.“Kwa upande wa Dar es Salaam Fomu za ushiriki pia zinapatikana jengo la SHAMO Tower, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam’’ alitaja.

Zaidi kuhusu usajili wa mbio hizo zinazoandaliwa kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA), Bidan alisema unaweza kufanyika kupitia tovuti ya kampuni hiyo ambayo ni www.capitalplus.co.tz

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »