Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias
Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS),
mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma wakati akikagua mashine ya kucharangia
mawe kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa
kiwango cha lami, mkoani Kigoma.
Mkandarasi
wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation Zhu Wan Li
akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (wa tatu kushoto), kuhusu
maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa
kiwango cha lami, mkoani Kigoma.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias
Kwandikwa akisikiliza maelezo ya Mhandisi Mkazi anayesimamia mradi wa
ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami kutoka
Kampuni ya DOCH Limited, Eng Mekbib Tesfaye, wakati akikagua ujenzi
wake, mkoani Kigoma.
Muonekano
wa sehemu ya barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa KM 63
inayojengwa kwa kiwango cha lami, ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia
asilimia 52, mkoani Kigoma.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias
Kwandikwa, akisikiliza maelezo kutoka kwa Eng. Raphael Ndimbo
(kushoto), katika chumba cha maabara ya mkandarasi wakati alipokuwa
akikagua ujenzi wa wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha
lami, mkoani Kigoma.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias
Kwandikwa (Mb), amewataka wananchi wanaopata nafasi za kazi katika
miradi ya ujenzi wa barabara kuwa wazalendo katika kulinda vifaa na
kuepuka vitendo vya hujuma vinavyoweza kujitokeza ili kuhakikisha miradi
hiyo inaenda kwa kasi na kumalizika kwa muda uliopangwa.
Mhe.
Kwandikwa ametoa kauli hiyo wilayani Kasulu mkoani Kigoma, alipokuwa
akikagua ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 inayojengwa na
mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation na
kuelezwa kuwa kuna wizi wa mafuta kiasi cha lita elfu 23 zilizoibiwa
hivi karibun ambapo amewataka wananchi kuwa na uzalendo kwanza katika
miradi yote ya ujenzi katika maeneo yote.
“Wizi
wa namna hii haukubaliki na mtandao ni mkubwa hivyo naagiza vyombo vya
usalama vichukue hatua kali mapema ili kuweza kuondoa madhara makubwa
zaidi”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Amewataka
makandarasi na wasimamizi wa miradi kutoa elimu kwa waajiriwa kila siku
kabla ya kuanza kazi kukemea tabia za wizi na ubadhilifu wowote
utakaowezea kutokea kwani ni moja ya sababu za miradi pia kuchelewa na
gharama kuongezeka.
Kuhusu
suala la ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha
lami Mhe. Kwandikwa, ameridhishwa na kasi ya ujenzi ya mkandarasi huyo
ambapo mpaka sasa maendeleo ya mradi umefikia asilimia 52.
Ameongeza
kuwa mkandarasi aendelee kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo kwa
kuwatengenezea barabara nzuri ya mbadala hasa kipindi hiki cha mvua ili
iweze kutumika kwa urahisi na kufanya wananchi kuendelea na shughuli zao
za kimaendeleo.
Aidha,
Mhe. Kwandikwa, amesisitiza kuwa nia ya Serikali ni kufungua mkoa wa
Kigoma kwa barabara za lami kwakuwa ni kiungo kikuu kwa nchi za Congo
DRC, Burundi na Rwanda na mkoa wenye uzalishaji mkubwa katika sekta ya
uvuvi, kilimo, madini na utalii.
Naibu
Waziri Mhe. Kwandikwa ametoa wito kwa madereva wote nchini kuzingatia
upakiaji wa mizigo kulingana na sheria na utaratibu waliopewa ili kuweza
kuzilinda barabara zetu nchini zinazojenga kwa fedha nyingi.
Kwa
upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma Eng.
Narcis Choma, amesema mradi wa ujenzi wa barabara hiyo utagharimu kiasi
cha shilingi bilioni 60 ambazo zote ni fedha za ndani na unatarajiwa
kukamilika mwezi Julai mwakani.
Ujenzi
wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami ukikamilika
utafungua fursa za ajira na uchumi na hivyo kuunganisha vizuri mkoa huo
na mikoa mingine ya nchi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
EmoticonEmoticon