TMA yatabiri msimu wa mvua za vuli mwezi Oktoba hadi Disemba 2017

September 04, 2017
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaoanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2017. Kushoto ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza Kabelwa akishiriki katika mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaoanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2017. Kushoto ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza Kabelwa pamoja na Mkurugenzi Matumizi ya Hali ya Hewa, Dk. Ladslaus Chang’a (kulia) wakishiriki katika mkutano huo.
Sehemu ya waandishi wa habari wakishiriki katika mkutano huo na TMA ikitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaoanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2017.

Sehemu ya waandishi wa habari wakishiriki katika mkutano huo na TMA ikitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaoanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaoanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2017. Kulia ni Mkurugenzi Matumizi ya Hali ya Hewa, Dk. Ladslaus Chang’a akiwa katika mkutano huo.
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaoanza mwezi Oktoba hadi Disemba 2017. Kwa mujibu wa taarifa ya utabiri iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi ambapo mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza Septemba, 2017 katika maeneo mengi ya Ziwa Viktoria na mwezi Oktoba, katika ukanda wa pwani, na baadaye mwezi Novemba katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki. 


Alisema ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2017 na hali kadhalika kutakuwa na vipindi virefu vya ukavu kujitokeza zaidi katika mwezi wa Oktoba, 2017.


Hata hivyo alisema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. 


Dk. Agnes Kijazi alibainisha kuwa mvua za chini ya wastani na vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza hususan katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na maeneo ya visiwa vya Unguja na Pemba.


"Pamoja na matarajio hayo ya mvua za wastani katika maeneo mengi ya nchi, uwezekano wa matukio ya vipindi vya mvua kubwa unatarajiwa hususan katika mwezi wa Disemba, 2017. Mtawanyiko hafifu wa mvua na vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo katika kipindi cha msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba, 2017 hususan katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kaskazini mwa mkoa wa  Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja and Pemba," alisema Mkurugenzi Mkuu.


Pamoja na hayo, Kijazi aliwashauri wakulima katika maeneo hayo kuandaa mashamba yao mapema na kupanda mazao yanayokomaa katika muda mfupi, huku akizitaka mamlaka husika, kama vile wadau wa Afya, menejimenti za maafa, Mamlaka za miji na wadau wengine kuchukua hatua stahiki katika kupunguza athari mbaya zinazoweza kutokea katika msimu wa mvua za Vuli 2017.


Aidha alisema kwa ujumala maeneo mengi yaliyopo kaskazini mwa nchi yanatarajiwa kupata mvua za wastani na uwezekano wa vipindi vifupi vya mvua kubwa hususan katika mwezi wa Desemba 2017.


Msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba (vuli) ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Kigoma). Na TMA inatarajia kutoa utabiri wa mvua katika maeneo mengine ya nchi yaliyosalia mwezi wa Oktoba 2017.

Imeandaliwa: wwwthehabari.com

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »