CCM YAPONGEZA UTEKELEZAJI WA ILANI KWA VITENDO KATIKA MANISPAA YA UBUNGO

September 05, 2017
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ubungo Ndg Salum A. Kalli akitoa salamu za CCM wakati wa uzinduzi wa Ugawaji wa vitambulisho vya awali 7296 vya matibabu Bure kwa Wazee katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam.
Zoezi la Uzinduzi wa Ugawaji wa vitambulisho vya awali 7296 vya matibabu Bure kwa Wazee katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ubungo kimetoa heko kwa viongozi wa serikali Wilaya ya Ubungo chini ya Mkuu wa Wilaya Mhe Kisare Makori kwa ushirikiano wake katika utendaji na kuipaisha Wilaya katika tathmini za mafanikio kwa wananchi wake ukilinganisha na ugeni wa Wilaya kwani ilianzishwa mwishoni mwa mwaka 2016.

Sambamba na Mkuu huyo wa Wilaya kwa ushirikiano mkubwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo sawia na watumishi wote wameifanya Manispaa ya Ubungo kuwa kwenye rekodi ya Manispaa zinazothamini wananchi wake hususani wazee.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ubungo Ndg Salum Kalli wakati wa uzinduzi wa Ugawaji wa vitambulisho vya awali 7296 vya matibabu Bure kwa Wazee katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam dhifa iliyofanyika katika viwanja vya TP Sinza E.

Kalli alitoa salamu za Chama hicho mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy A. Mwalimu ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambaye pia Mhe Ummy aliahidi kutoa Bima za afya kwa watoto 100 wenye umri chini ya miaka 18 waishio katika mazingira magumu sambamba na kujenga wodi ya wazazi, watoto na maabara ya damu kwenye kituo kimoja cha afya.

Alisema kuwa uzinduzi huo wa ugawaji wa vitambulisho ni kuonesha umma wa watanzania kuwa Wilaya ya Ubungo inawajali Wazee ikiwa ni Sehemu ya utekelezaji wa ilani ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi katika kipindi Cha mwaka 2015-2020.

Alisema kuwa katika Sura ya nne, ibara ya 50 (P) inaeleza kuwa Halmashauri zitahakikisha wazee wanatambuliwa na kupewa matibabu bure katika Hospitali za serikali hivyo Manispaa ya Ubungo imetekeleza mkataba wa CCM na wananchi kwa vitendo ndani ya miaka miwili kabla ya kumalizika miaka mitano ya ahadi.

Kalli alisema kuwa pamoja na jambo hilo pia Wilaya ya Ubungo inapaswa kusimama kidete katika shughuli zingine mbalimbali ili kuwaletea maendeleo wananchi kutokana na imani kubwa walioionyesha Octoba 25, 2015 kwa kutoa ridhaa kwa Chama Cha Mapinduzi.

Kalli aliahidi mbele ya wahudhuriaji wa dhifa hiyo kuwa CCM itaendelea kuwaletea maendeleo wananchi huku akimpongeza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jackobo kwa kuiishi na kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo.

“Mgeni rasmi naahidi mbele ya hadhara hii kuwa CCM tutaendelea kuja mara kwa mara katika ofisi za serikali kukagua utekelezaji wa ilani ya ushindi mahali tutakapobaini kuwa ilani haitekelezwi tutakemea vikali kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla wake”
Wilaya ya Ubungo imekuwa Walaya ya pili katika Jiji la Dar es salaam kutekeleza agizo la serikali lililotolewa na Waziri Mkuu kwenye maadhimisho ya siku ya Wazee Octoba 1, 2009 kuwa Hospitali zote na Vituo vya Afya vya Umma kutenga dirisha na watumishi maalumu wa Afya kwa ajili ya kutoa Huduma za matibabu bure kwa Wazee.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »