Na: Judith Mhina – MAELEZO
Hakika
historia imejirudia, mkoa wa Tanga ni kati ya mikoa mashuhuri nchini
Tanzania kabla ya uhuru wa Tanganyika katika kupigania uhuru, kwa kuwa
ni mkoa uliokuwa na wasomi wengi kuliko mikoa mingine wakati huo.
Hii
ilitokana na uwepo wa shule za wamisionari wa kanisa la Anglikana (UMCA)
ambalo ni la kwanza kuingia katika Pwani ya Afrika Mashariki mwaka 1878
na waliojenga shule za Magila na Kiwanda Muheza, Korogwe misheni,
Kideleko Handeni (Shule za Kati) na Saint Andrew Minaki Pwani (shule ya
Sekondari).
Hata
baada ya uhuru chini ya Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili ya
uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere na Rais
Msataafu Ali Hassan Mwinyi, mkoa wa Tanga ulikuwa maarufu kutokana na
uwepo wa viwanda vingi, njia za reli na Bandari yenye kina kirefu yenye
uwezo wa kuingiza meli kubwa za mizigo za Kitaifa na Kimataifa.
Viwanda
ambavyo vilijengwa katika mkoa wa Tanga ni pamoja na vya chuma, mbolea,
saruji, maziwa, kamba za katani na mazulia, amboni plastic, mbao,
sabuni maarufu ya mbuni, gardenia, foma na mafuta ya nazi.
Historia
hii sasa inajirudia katika mkoa wa Tanga baada ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, kupigania kwa nguvu zote
Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja nchini Tanzania
ambalo litaishia katika kijiji cha Chongoleani.
Wananchi
wote wa Tanzania wana kila sababu ya kujivunia ujenzi wa bomba hilo la
mafuta ambalo litawapatia ajira Watanzania hususan wananchi wa mkoa wa
Tanga. Pongezi kubwa ziende kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli kwa juhudi zake za kuhakikisha kwamba Mradi huu unakuja
Tanzania. Wananchi wa mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla wana kila
sababu ya kulinda heshima ya nchi yetu kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo
na ulinzi mkali wa Bomba hilo kila mahali lilikopita.
Kurejea
kwa mkoa wa tanga katika ramani ya Tanzania ya viwanda umedhihirishwa
na Wananchi wa Chongoleani ambao siku ya uwekaji jiwe la msingi walikuwa
wawakilishi wa Watanzania ambao hawakupata fursa ya kwenda Tanga
kumshuhudia Mheshimiwa Rais na na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda
Yoweri Kaguta Museveni wakifungua pazia la jiwe la msingi kuashiria
uzinduzi wa Mradi huo.
Kutokana
na tukio hilo la uwekaji wa jiwe la msingi wana Chongoleani walitoa ya
moyoni kwa kuonyesha furaha yao isiyo na kifani kupitia kwa Mwenyekiti
wao wa kijiji Ndugu Mbwana Nondo wakisema; “Kwa moyo wa dhati kabisa
tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutujali
Wananchi wake kwa kutuletea neema ya mradi huu wa bomba la mafuta”.
Aidha,
Mwenyekiti huyo aliongeza kwa kusema kwamba, katika maisha yetu
Wananchi wa Chongoleani hatutaweza kumsahau Mheshimiwa Rais kwa mambo
mengi anayowafanyia Watanzania na Taifa kwa ujumla na itakuwa ni
kumbukumbu kwa kizazi kijacho.
“Napenda
kusisitiza kwamba tunamuahidi Rais, kuwa wote watakaopata fursa kwenye
Mradi huu wa Bomba la Mafuta, watafanyakazi kwa bidii ili kujiletea
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”. Alihitimisha Bw
Nondo.
Naye
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Bibi Ummy
Mwalimu, amewaomba wanawake wa Mkoa wa Tanga kuchangamkia fursa
zinazojitokeza, kutokana na uwepo wa mradi wa bomba la mafuta.
Akisisitiza
kuhusu ajira hizo amesema; “Kwa wale wenye ujuzi wanaweza kupata ajira
za kudumu katika mradi, ila kwa wale ambao hawana ujuzi wachangamkie
fursa nyingine kama mama lishe ambapo mkoa unjulikana kwa kujua kupika
mapishi yanayovutia walaji wengi”
Aidha,
amewaasa wakulima kuona fursa ya kulima mazao ambayo yataliwa kwa wingi
kwa watumishi watakaoajiriwa Tanga katika mradi wa bomba la mafuta.
Mfano matunda na mbogamboga ambavyo ni sehemu ya kuimarisha lishe za
watumishi hao watakao kaa Tanga.
Mradi
wa Bomba la Mafuta ni ishara njema kwa Watanzania, Serikali na Taifa kwa
ujumla maana inaonyesha dhahiri kukosekana kwa fursa kama hii kwa miaka
mingi katika mkoa wa Tanga ni fundisho kwa Watanzania hususan Wananchi
wa mkoa wa Tanga kama waswahili wasemavyo “usichezee shilingi chooni”
ikiwa na maana shilingi ikitumbukia kuipata sio rahisi.
Kila
jambo jema lina fursa zake, nalo bomba la mafuta limekuja na neema zake,
mfano wana Chongoleani kupata barabara ya kilometa 8 inayowaunganisha
na barabara kuu ya kutoka Tanga kwenda Horohoro. Hii ina maana kubwa kwa
wana chongoleani kiuchumi, maana watakuwa na wepesi wa usafiri wa
mabasi na malori. Hivyo, bidhaa zitokazo chongoleani sasa zitaenda Tanga
na nje ya mkoa wa Tanga kwa urahisi. Mfano samaki, mazao ya chakula na
mengineyo.
Wafanyabiashara
wetu wachangamkie fursa iliyojitokeza watembelee eneo husika na
kudadisi kipi wanachoweza kufanya biashara kwa ajili ya kuinua kipato
chao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Kama
tujuavyo Taifa letu liko kwenye harakati za kuelekea katika uchumi wa
viwanda, na kama ujuavyo Tanga ni Mkoa wenye kuzalisha matunda ya aina
mbalimbali na mbogamboga kwa wingi, nazi, katani, mahindi, viazi,
maharagwe, samaki, viungo kama tangawizi, iliki, pilipili manga,
mdalasini, chai na mifugo kama ngombe mbuzi na kondoo wapo kwa makundi
katika ranchi zinazotambulika na wale wanaofugwa kiasili.
Katika
suala zima la bomba la mafuta ni muhimu mikoa yote ambapo bomba
linapita kutambua na kujiandaa kuitumia fursa zilizopo na zitakazo
jitokeza katika mikoa ya; Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida,
Dodoma Morogoro na Tanga. Wilaya zitakazopitiwa na bomba hilo zipo 24 na
vijiji zaidi ya 180, vitafahamishwa kwa usahihi hapo baadaye.
Kwa
kuwa Wizara ya Nishati na Madini inahamasisha kwa pamoja na wadau
mbalimbali ni vema kutumia mafunzo hayo, kujiimarisha na kuwa sehemu ya
matokeo mazuri ya bomba husika.
Bomba
la Mafuta la kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga Chongoleani lina urefu wa
Kilometa 1445 ambapo kwa upande wa Tanzania itakuwa na jumla ya kilometa
1115 na Uganda 330. Aidha, Mradi utatarajia kusafirisha mapipa laki
mbili na kumi na sita elfu (216,000) kwa siku .
Kijiji
cha Chongoleani ndio kituo cha mwisho ambapo mitambo mikubwa itasimikwa
katika eneo hili kwa ajili ya kusukuma mafuta eneo la baharini ili,
kuweka kwenye vyombo vya usafirishaji kusafirisha maeneo mbalimbali
duniani ambayo Uganda watakuwa wamepata soko.
Tanzania
itafaidika na mradi huu kutokana na kodi, tozo na mrahaba wa bomba la
mafuta, itakayofanywa moja kwa moja na mradi huo. Faida nyingine ambazo,
sio za moja kwa moja ni ajira, fursa za kufanya biashara katika mikoa 8
ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro
na Tanga.
Tusisahau
unapopata fursa moja, ni vema kuitumia kwa kuimarisha na kuitangaza
Tanga kimataifa kwa upande wa utalii katika machimbo ya Amboni, utalii
wa samaki adimu duniani Silikanti eneo la ufukwe wa Kigombe. Samaki huyu
alikuwepo duniani miaka 6000 iliyopita, ambapo alitoweka na kugundulika
kuwa yupo katika pwani ya bahari ya hindi eneo la Kigombe Muheza Tanga.
Aidha,
utalii wa milima ya Usanbara na Nnguu Kilindi, misitu ya asili ambayo
kama vile miti ya miwati inayotengeneza nta au gundi, Tao la Mashariki
misitu ya asili ya Nguu na maporomoko ya maji katika Tao la mashariki
ikiwa ni pamoja na milima ya usambara, amani, maghamba, na nguu. Uoto wa
asili na baridi ambayo isingedhaniwa kabisa kuwepo katika milima
inayoelekea bahari ya Hindi.
Pia
Hifadhi ya Taifa ya wanyamapori ya Saadani yenye kivutio cha ngiri
wanaoishi katika makazi ya binadamu ambayo ni mbuga pekee iyopo
pembezoni mwa bahari katika Afirka mashariki, pia mbuga ya Mkomazi na
mbuga ya uwindaji wanyapori ya Nnguu, madini ya aina mbalimbali, Kasa wa
pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi na vipepeo adimu duniani wa
milima ya usambara Amani. Ni vema kuwakarimu wageni kwa utamaduni wa
asili wa Tanga kwa kuwaonyesha mapishi na ukarimu uliotukuka wa
Watanzania wapatapo wageni.
Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.
Chanzo:Michuzi Blog
EmoticonEmoticon